Waislam wengi kote duniani walishtumu vikali mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa Septemba 11 mwaka wa 2001 nchini Marekani. Lakini wengi wanaona hatua zilizochukuliwa na Marekani kufuatia mashambulizi hayo kuwa hatua mbaya zaidi. Vita vilivyofuatia vya Afghanistan na Iraq na sasa kuingiliwa kati kwa Libya na majeshi ya muungano wa NATO. Pamoja na hilo kuungwa mkono kwa tawala zinazodai kuwa zinatishiwa na ugaidi, huku zikisingizia upinzani.
Mchanganyiko wa mambo haya hugubika juhudi za Marekani za ukombozi na uungaji mkono wake wa tawala za kidemokrasia anasema Steven Kull mkurugenzi wa taasisi ya kimataifa ya maswala ya Sera katika chuo kikuu cha Maryland hapa Marekani.
Maoni ya waislamu miaka 10 baada ya Sept 11
“Kuna hisia kuwa kuna Marekani, ambayo haitekelezi inachosema ni cha thamani kwake na inayoonekana kuwa adui wa Uislam, iliyo tayari kutumia nguvu za kijeshi bila kujali sheria za kimataifa na kuunga mkono demokrasia.”
Esam El Erian, kiongozi wa kundi la Muslim Brotherhood nchini Misri naye anasema operesheni za kijeshi za Marekani zimeuwa watu wengi zaidi kuliko mashambulizi ya kigaidi na kwamba kutumia nguvu kuleta uthabiti na kushinikiza utawala wa kidemokrasia katika nchi za Kiislam ni juhudi zilizoshindikana.
“ Walishindwa nchini Afghanistan? Ndiyo. Walishindwa kukarabati upya nchi hiyo. Walishindwa nchini Iraq? Ndiyo. Walishindwa kujenga taifa la kidemokrasia…”
Kura za maoni zinaonyesha kuwa juhudi za rais Barack Obama kushirikisha dunia ya waislam hazijakuwa na mafanikio ya maana katika hisia kama hizi. Lakini Indonesia ina maoni tofauti juu ya Marekani. Ukweli kwamba kwa wakati mmoja rais Obama utotoni mwake aliishi nchini humo; kwamba Indonesia imepata pigo kutokana na mashambulizi ya kigaidi na kwamba imefanya mabadiliko kadha kuelekea katika utawala wa kidemokrasia, unaeleza kwa nini Indonesia inaonekana kuipendelea Marekani. Lakini hata hivyo kuna baadhi ya raia nchini humo wanaokemea vikali sera za kijeshi za Marekani , na ushirika wake na Israel. Mwaka jana Israel ilisababisha maafa makubwa pale iliposhambulia msururu wa meli za msaada na kuzusha maandamano makali mjini Jakarta. Mwanafunzi wa chuo kikuu cha Indonesia Sahid Sundana anasema:
“Rais Obama anapaswa kuzuia Israel kufanya kitendo kama hicho, na isiilinde wala kuistiri Israel”
Nchini Tunisia, wengine wanashtumu Marekani kwa kutotoa msaada wa kutosha kwa makundi ya wanaharakati wa kidemokrasia, lakini kwa raia huyu, anahisi kuna mabadiliko kiasi katika sera za Marekani.
“ Wamarekani wameanza kuonyesha ushirika wao kiasi na Tunisia, na hata kuwa wakarimu, ninadhani wataisadia Tunisia na wameanza kufanya hivyo….”
Kull anasema Marekani inapaswa kuwa mshirika katika harakati za demokrasia zinazoibuka katika dunia ya waislam, na kwamba inahitaji kuunda urafiki zaidi na nchi hizo vinginevyo itaendelea kuchukuliwa na nchi hizo kwa hisia mchanganyiko.
Miaka 10 imepita tangu magaidi kushambulia Marekani Septemba 11 mwaka wa 2001 lakini hisia za waislam juu ya Marekani zimekwama kati ya kile kinachoitwa vita dhidi dhidi ya ugaidi .