Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Aprili 15, 2024 Local time: 02:32

Malawi yasema itatoa chanjo ya kwanza ya malaria barani Afrika


Mtoto katika kijiji cha Tomali nchini Malawi akipewa chanjo ya kwanza duniani dhidi ya malaria, kutokana na mradi wa majaribio.
Mtoto katika kijiji cha Tomali nchini Malawi akipewa chanjo ya kwanza duniani dhidi ya malaria, kutokana na mradi wa majaribio.

Wizara ya afya ya Malawi inasema hivi karibuni itatoa chanjo ya kwanza ya malaria barani Afrika kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Chanjo ya RTS,S, ambayo ilijaribiwa nchini Ghana, Kenya, na Malawi, ilichukua zaidi ya miaka 30 kutengenezwa.

Wakati chanjo hiyo ina kiwango cha chini cha ufanisi, imeibua matumaini ya kuokoa watu zaidi ya 400,000 wanaofariki kila mwaka, kutokana na ugonjwa huo, unaoenezwa na mbu, wengi wao wakiwa watoto wa Kiafrika.

Utoaji wa chanjo, uliopangwa kufanyika mwezi ujao, unafuatia kukamilika kwa awamu ya majaribio. Tangu mwaka 2019, Shirika la Afya Ulimwenguni limechanja watoto 360,000 kwa mwaka nchini Malawi, Ghana na Kenya, na theluthi moja yao nchini Malawi.

Khumbize Kandodo Chiponda ni waziri wa afya wa Malawi alisema uamuzi huo umefikiwa kufuatia majadiliano ambayo Rais wa Malawi Lazarus Chakwera alikuwa nayo na wawakilishi wa PATH, shirika lisilo la kiserikali la afya duniani, alipohudhuria mkutano wa mwaka huu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.

WHO iliidhinisha chanjo hiyo miaka kadhaa iliyopita ikisema ni mafanikio katika vita dhidi ya malaria.

Chanjo hiyo, inayouzwa na kampuni ya GlaxoSmithKline kama Mosquirix, inafanya kazi kwa takriban asilimia 30 na inahitaji dozi nne.

Hata hivyo, Wakfu wa Bill na Melinda Gates, waungaji mkono wa chanjo hiyo, wameibua wasiwasi ikiwa chanjo hiyo inalingana na thamani ya gharama iliyotumika.

Mwezi Julai, The Associated Press ilimnukuu Philip Welkhoff, mkurugenzi wa programu za malaria wa Wakfu wa Gates, akisema Wakfu hautatoa tena usaidizi wa moja kwa moja wa kifedha kwa chanjo hiyo ingawa itafadhili muungano unaounga mkono chanjo hiyo.

Alisema chanjo ya malaria ina ufanisi mdogo kuliko wanavyotaka na kwamba chanjo hiyo ni ghali kiasi na ina changamoto ya utoaji.

Maziko Matemba ni mwanaharakati wa afya na balozi wa afya ya jamii nchini Malawi anasema hakuna haja ya kuwa na wasiwasi juu ya ufanisi wa asilimia 30, akisema sio chanjo zote zina ufanisi wa asilimia 100.

Takwimu zinaonyesha kuwa Malaria ndio ugonjwa unaoua zaidi nchini Malawi. Ugonjwa huu huchangia asilimia 36 ya wagonjwa wote wa nje wa hospitali na asilimia 15 ya wanaolazwa hospitalini.

Licha ya kiwango cha chini cha ufanisi wake, baadhi ya wanasayansi wanasema chanjo hiyo itakuwa na athari kubwa dhidi ya malaria barani Afrika, ambayo inarekodi visa milioni 200 na vifo 400,000 kwa mwaka.

XS
SM
MD
LG