Majeshi yanayotii serikali mpya ya umoja wa kitaifa mjini Tripoli yameripotiwa kuongeza nguvu ndani ya pwani ya mji wa Sirte unaoshikiliwa na kundi la Islamic State huku vikosi vinavyotii serikali ya upinzani mjini Tobruk vinasema wamewarudisha nyuma wanamgambo wa al-Qaida huko Benghazi.
Wanamgambo wanaotii serikali ya umoja wa kitaifa walikamata wilaya mbili ndani ya Sirte kufuatia mapigano makali na kuripotiwa kutokea vifo kwa pande zote mbili.
Ahmed Hadiya, msemaji wa vikosi vya wanamgambo wanaounga mkono serikali huko Sirte aliiambia televisheni ya Libya kwamba mapambano yalifanyika katika maeneo kadhaa.
Anaongeza kusema kwamba wanamgambo wanaounga mkono serikali waliwasukuma wapiganaji wa IS nje ya wilaya za Zafran na Gharbiyat na kisha kuwaweka kati wanamgambo hao katika maeneo madogo yenye mitaa 700 na kituo cha mkutano cha Ouagadougou.
Wapiganaji wa Islamic State waliripotiwa kufanya mapambano makali licha ya kupoteza udhibiti hivi karibuni wakitumia mabomu ya kutegwa ndani ya gari, washambuliaji wa kujitolea mhanga na vifaa vingine vinavyosababisha milipuko ya mauaji.
Kamanda wa wanamgambo wa serikali huko Sirte aliwaambia waandishi wa habari kwamba wapiganaji wa Islamic State-IS walikuwa na magari yaliyokuwa na vilipuzi vya mauaji na walikuwa na nia ya kusitisha serikali kusonga mbele kuingia ndani ya mji.
Gazeti la Libya Herald liliripoti kwamba wanamgambo 170 wanaounga mkono serikali wameuwawa na zaidi ya 700 walijeruhiwa tangu kuanza kwa operesheni ya kijeshi ya kuuteka tena mji wa Sirte.