Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 13, 2024 Local time: 06:02

Majambazi waliovamia kituo cha polisi stakishari wakamatwa


Polisi wa kutuliza ghasia wakishirikiana na polisi wa kawaida katika matukio mbali mbali ya uhalifu
Polisi wa kutuliza ghasia wakishirikiana na polisi wa kawaida katika matukio mbali mbali ya uhalifu

Jeshi la polisi nchini Tanzania lilisema kwa sasa limebadili mfumo wake wa kupambana na uhalifu baada ya kubaini kwamba kuna kundi la kihalifu limeibuka nchini humo linalotumia mbinu za hali ya juu za kuteka vituo vya polisi, kuua askari polisi na kupora silaha.

Kauli hiyo ya jeshi la polisi ilitolewa Jumatatu na kamanda wa polisi kanda maalum Dar es Salaam, Bwana Suleiman Kova muda mchache baada ya kutangaza kuwakamata watuhumiwa watano wa ujambazi wanaodaiwa kuhusika na uporaji wa silaha katika tukio lililotokea hivi karibuni kwenye kituo cha polisi cha Stakishari cha jijini Dar es Salaam ambapo askari polisi wanne na raia watatu waliuwawa pamoja na silaha kadhaa kuporwa.

Katika msako huo watuhumiwa watatu wameuwawa na wengine wawili wanahojiwa huku silaha zilizokamatwa zikiwa 14 na risasi 28 zote zilizoporwa kwenye kituo cha Stakishari huku silaha mbili zaidi zilikutwa kwa watuhumiwa hao waliokutwa mafichoni huko mkoani Pwani.

Ingawa kamanda Kova hakutaka kuhusisha moja kwa moja matukio hayo na ugaidi lakini alikiri kwamba ni wahalifu wanaotumia mbinu ya aina tofauti na iliyoandaliwa vyema.

Kamanda Kova alilisifia jeshi la polisi kwa juhudi zake katika operesheni iliyofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na silaha walizokutwa nazo.

Kwa mujibu wa jeshi la polisi watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa wameficha silaha hizo nje ya nyumba moja ya ibada huko mkoani Pwani.

Ripoti ya Dina Chahali, Dar Es Salaam, Tanzania
please wait

No media source currently available

0:00 0:02:31 0:00
Kiungo cha moja kwa moja

XS
SM
MD
LG