Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 04:17

Majaji waliokataliwa na Kenyatta wameapishwa na utawala wa Ruto


Rais wa Kenya Dr. William Ruto akiwa na jaji mkuu Martha Koome mda mfupi baada ya kuapishwa jijini Nairobi, Kenya. Sept 13 2022. Picha: Reuters
Rais wa Kenya Dr. William Ruto akiwa na jaji mkuu Martha Koome mda mfupi baada ya kuapishwa jijini Nairobi, Kenya. Sept 13 2022. Picha: Reuters

Rais wa Kenya Dr. William Ruto ameongoza hafla ya kuapishwa kwa majaji sita wa mahakama ya rufaa, mazingira na ardhi ambao rais aliyeondoka madarakani Uhuru Kenyatta alikataa kuwateua kutokana kile kilitajwa kama “uadilifu wao unaotiliwa shaka”.

Katika hafla ambayo pia imehudhuriwa na aliyekuwa Jaji mkuu David Maraga ambaye alikuwa na uhusiano mbaya na Kenyatta, Rais Ruto ameiomba Idara ya Mahakama kushirikiana na serikali yake na kuwawezesha Wakenya kupata haki kwa haraka.

Ruto anasema serikali yake itazingatia utawala wa kisheria na heshima kwa taasisi huru.

Hafla hiyo imefanyika siku moja baada ya Ruto kuapishwa kuwa rais wa tano wa jamhuri ya Kenya.

Hii ni sehemu ya sehemu ya kutimiza ahadi mojawapo za kampeni za kisiasa alizotoa hapo awali.

Majaji sita walioapishwa ni Professa Joel Ngugi, George Odunga, Weldon Korir, Aggrey Muchelule, hakimu mkuu wa mahakama kuu Evans Makori na Msajili wa mahakama hiyo Judith Omange.

Kenya alikataa kuidhinisha uteuzi wa majaji hao

Kenyatta aliwatenga sita hao lakini baadaye tume ya Huduma za Mahakama nchini Kenya ilifanya mchakato mwingine uliofanikisha kuapishwa kwa majaji wengine saba wanaojumuisha Majaji wa Mahakama Kuu Luka Kimaru Kiprotich, Lydia Awino Achode, John Mativo Mutinga, Abida Ali Aroni, Frederick Ochieng’ Andago, Ngenye Grace Wangui na wakili Paul Gachoka Mwaniki.

Danstan Omari ambaye ni wakili wa mahakama kuu nchini Kenya anaeleza kuwa hatua hii ni afueni kwa mahakama ya rufaa ambayo inakabiliwa na mrundiko mkubwa wa kesi zinazohitaji usuluhishi wa kasi.

Omari vile vile anaeleza kuwa kuteuliwa na kuapishwa kwa majaji hawa ni hatua za kujaribu kuondoa doa lililogubika utawala wa Kenyatta, unaotajwa kutozingatia utawala wa kisheria.

Jaji George Vincent Odunga, mwenye umri wa miaka 54, alikuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Machakos.

Kuwahusu majaji walioapishwa

Na zamani alikuwa Jaji katika Kitengo cha Biashara na Kitengo cha Kiraia na Jaji Kiongozi, Kitengo cha Mapitio ya Mahakama.

Jaji Weldon Korir, mwenye umri wa miaka 56, kuanzia Agosti 2011 amekuwa Jaji wa Mahakama Kuu; na kati ya mwaka 2021 na Septemba 2022 kabla ya uteuzi huu, amekuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Kapenguria. Pia amewahi kuhudumu kuwa Jaji Kiongozi, Kitengo cha Katiba na Haki za Kibinadamu kuanzia.

Jaji Professa Joel Ngugi,mwenye umri wa miaka 50, amekuwa akihudumu kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Kenya na pia amekuwa akihudumu kuwa Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Nakuru na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Uendeshaji ya Utekelezaji wa Sera ya Mifumo Mbadala ya Haki.

Kutoka mwaka 2009 hadi sasa, Jaji Aggrey Muchelule, mwenye umri wa miaka 65, amekuwa akihudumu kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Kenya. Pia amewahi kuhudumu kuwa jaji kiongozi wa mahakama kuu za Nairobi, Kisii, Embu, Bungoma na Kisumu na hadi uteuzi wake amekuwa akihudumu katika Idara ya Familia jijini Nairobi kama Jaji Kiongozi.

Evans Makori mwenye umri wa miaka 52, ambaye ameteuliwa kuwa hakimu wa mahakama ya mazingira na ardhi, amekuwa akihudumu kuwa Hakimu Mkuu na Mkuu wa Kituo cha Mahakama za Kericho huku jaji Judith Omange mwenye umri wa miaka 49 ambaye ameteuliwa kuwa jaji wa mahakama hiyo ya mazingira na ardhi, amekuwa akihudumu kuwa Msajili wa Mahakama kuu nchini Kenya.

Wachambuzi wanasemaje kuhusu kuapishwa kwa majaji?

Professa Hezron Mogambi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi, anaeleza kuwa hili linaashiria mwamko mpya wa mahusiano kati ya tawi kuu la serikali linaloongozwa na rais na idara ya mahakama nchini Kenya.

Hafla hiyo iliyoongozwa na Msajili wa mahakama nchini Kenya Anne Amadi, imehudhuriwa na Jaji Mkuu Martha Koome na majaji wote walioteuliwa na rais aliyeondoka mamlakani, Uhuru Kenyatta.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi

XS
SM
MD
LG