Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Oktoba 05, 2022 Local time: 08:04

Maiti 421 zagunduliwa ndani ya kaburi moja huko DRC


Mfano wa moja ya kaburi lililozikwa watu wengi kwa pamoja

Mjadala mkali umezuka huko Kinshasa kufuatia kuzinduliwa kwa kaburi la pamoja ambalo lilizika watu 421 nje ya mji wa Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC.

Serikali ilielezea kwamba maiti zilizozikwa humo nyingi ni za watoto wachanga waliofariki wakati wa kuzaliwa kwenye mahospitali kadhaa pamoja na watu wazima ambao familia zao kwa kipindi kirefu walishindwa kugharamia mazishi. Lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu yaliomba uchunguzi huru ufanyike ilikufahamu idadi kamili na sababu za vifo vya watu hao.

Viongozi wa mji wa Kinshasa walitupilia mbali madai ya watu kwamba maiti 421 zilizozikwa mtaani huko Maluku kilomita 100 kutoka mji wa Kinshasa ni za wapinzani wa serikali. Kwenye mkutano na waandishi habari, Robert Luzolanu, meya wa muda wa mji wa Kinshasa alisema kwamba hawana chochote cha kuwaficha wananchi wa Kongo juu ya tukio hilo.

“Mazishi ya pamoja ya maiti hao ni kama desturi ya viongozi wa mji wa Kinshasa, kila mara wakati chumba kikuu cha kuwekea maiti kinapo jaa na maiti ya watoto wachanga waliofariki wakati wa kuzaliwa kwao na watu ambao hawana familia hapa Kinshasa, tunatoa amri kwa wizara inayohusika na maswala ya jamii kuandaa nafasi ya kuzikwa kwa maiti hao. Hatuna cha kuficha kulikuwa na watu 421 waliozikwa huko Maluku, kwenye makaburi yaitwayo FULAFULA na tulifanya hivyo kama kawaida yetu”.

Aliendea kusema kwamba mwaka uliopita maiti wengine 382 walizikwa kwenye makaburi hayo.Wengi wao wakiwa ni watoto waliozaliwa ama mimba zilizotoka.

Ramani ya DRC
Ramani ya DRC

Maelezo hayo ya maafisa wa serikali yamekuja baada ya mashirika ya kiraia na wabunge wa upinzani kulazimisha uchunguzi wa kina kufanyika ilikufahamu idadi na aina ya watu waliozikwa huko Maluku. Tayari waziri wa mambo ya ndani huko Kongo ametakiwa kujieleza bungeni kuhusu tukio hilo. Lakini siku ya kujieleza kwake bado haijatangazwa kutokana na kwamba spika wa bunge yupo nje ya nchi kwa ziara ya kikazi.

Mbunge wa upinzani Toussaint Alonga aliiomba serikali kutoa ufafanuzi haraka iwezekanavyo kuhusu tukio hilo. “Ni kwa faida ya serikali kutupa maelezo ya kweli kuhusu kaburi hilo la pamoja na ikiwa haitofafanua vyema tukio hilo basi ni majukumu yetu sisi kama wabunge kutafuta ukweli”.

Shrika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch- HRW lilisema huenda maiti zilizozikwa kwenye kaburi hilo zikawa za watu waliouliwa wakati wa maandamano ya kupinga mageuzi ya sheria ya uchaguzi mapema mwaka huu ama wakati wa operesheni ya polisi dhidi ya magenge ya ujambazi mjini Kinshasa hapo mwaka jana. Umoja wa Mataifa ulielezea kwamba tayari umepata taarifa kuhusu kilicho tokea nchini humo na tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa nchini Kongo-MONUSCO kupitia ofisi yake ya haki za binadamu ilieleze kwamba maafisa wa sheria wa Kongo waliwasiliana nao kwa ajili ya ushirikiano katika kufafanua tukio hilo.

XS
SM
MD
LG