Umoja wa Ulaya mwezi Machi mwaka jana, uliamua kuondoa vikwazo ulivyomuwekea Mubarak, mke wake, na watoto wake wawili wa kiume na wake zao, kufuatia maandamano makubwa ya Januari 2011 ambayo yalimaliza utawala wa miaka 30 wa Mubarak.
Vikwazo hivyo vilikuwa pamoja na kufungiwa kwa mali za Mubarak zinazoshikiliwa katika Umoja wa Ulaya na kuweka marufuku kwa raia au taasisi kutoka Jumuia hiyo ya nchi wanachama 27 kutoa ufadhili kwa wanafamilia wa Mubarak waliowekewa vikwazo.
Hatua hizo zilichukuliwa kusaidia viongozi wa Misri katika kurejesha mali za serikali zilizoporwa.
Lakini uamuzi wa Jumatano umeeleza kuwa “ kuendelea kutekeleza vikwazo hivyo” hakutakuwa na maana yoyote inayoeleweka.
Mbali na kuipa fursa familia ya Mubarak kupata fedha zilizokuwa zimezuiliwa, mahakama hiyo iliamuru Baraza la Umoja wa Ulaya kulipa ghamara zilizotumiwa na familia yake.
Mubarak na familia yake walipinga mara kadhaa hatua hizo za adhabu mahakamani, na kusababisha mapambano ya kisheria yaliyodumu muongo mmoja.
Mubarak alifariki mwaka wa 2020 akiwa na umri wa miaka 91.