Kufuatia tamko la rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, kupunguza mishahara ya wakuu wa taasisi na mashirika ya umma nchini Tanzania baadhi ya wachambuzi wamepokea kwa hisia tofauti nchini humo.
Uamuzi huo utaathiri mashirika mengi ya umma nchini humo ambapo baadhi ya wakuu wake wametajwa kupokea mshahara wa zaidi ya milioni 30 kwa mwezi .
Mchambuzi wa siasa nchini Tanzania na mhadhiri wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo, anasema kufanya kazi kwenye mashirika haya ni sehemu ya utumishi wa umma na akisistiza kwamba wakuu wa mashirika haya wasitarajie kulipwa kiasi kikubwa kupita kiasi akipinga wale wanaodai kwamba kupunguza mishahara hiyo kunaweza kupunguza utendaji au morali katika mashirika ya umma.
Pia akiongeza kwamba ili Rais Magufuli na chama chake wafanikiwe lazima wabadilishe mtazamo wa kisera, kiitikadi na kifalsafa bila hivyo mabadiliko hayatakuwa na msingi wowote wa kufanikiwa.