Rais Ramaphosa amesema katika hotuba kupitia televisheni ya taifa “ Hili ni janga la kibinadamu ambalo linahitaji juhudi kubwa na za haraka za kutoa msaada.”
“Maisha, afya na ustawi wa maelfu ya watu bado vipo hatarini,” ameongeza.
Ramaphosa amesema “Bandari ya Durban ambayo ni mojawapo ya vituo vikubwa na vyenye shughuli nyingi za meli katika bara hili na ambayo ni muhimu kwa uchumi wa nchi imeathirika vibaya.”
Watu 443 walifariki, 48 hawajulikani walipo, kando na mji wa pwani ya mashariki wa Durban, rais amesema.
Ameongeza kuwa bado ni tatizo kufika kwenye baadhi ya maeneo yaliyoharibiwa vibaya, zikiwemo shule 16 ambazo zimeteketea kabisa.
Hali ya janga, sawa na hatua zilizowekwa kupambana na janga la Covid 19, inahitaji uwezo wa kifedha wa ziada kusaidia katika ukarabati wa vilivyoharibika.
Ili kuondoa hofu kuhusu ufisadi ambao ulizorotesha juhudi za kupambana na Covid, Ramaphosa amesema serikali itaunda taasisi maalum ya uangalizi itakayojumuisha mkaguzi mkuu wa hesabu, wafanyabiashara na makundi ya kidini, pamoja na mashirika ya kitaaluma ya wahandishi na wahasibu.