Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 16:23

Maendeleo yapatikana katika malengo ya millennia.


Katibu mkuu wa umoja mataifa Ban Ki Moon, amesema Jumatano kuwa, japo kuna mizozo ya kimataifa ya chakula, nishati, na fedha, kumekuwa na maendeleo katika mkutano wa malengo ya maendeleo ya millennia au MDG’s ya kupunguza umasikini kwa nusu ifikapo mwaka 2015.

Katibu mkuu Ban ki Moon, alisema hali ya uchumi isokuwa na uhakika haiwezi kuwa sababu ya kupunguza juhudi za maendeleo, lakini ni sababu ya kuyaharakisha.

“Kwa kuwekeza katika maendeleo ya milenia, tunawekeza katika kukuza kwa uchumi wa ulimwengu. Kwa kulenga juu ya mahitaji ya wale walodhaifu zaidi, tunaweka misingi ya mafanikio na ustawi wa kesho.” alisema Bw. Ban Ki Moon.

Bw. Ban alisema kumekuwa na maendeleo makubwa katika kuwafanya watoto kuingia shule za msingi huko kusini mwa jangwa la Sahara la Afrika, na kuboresha afya ya mtoto na usawa wa kijinsia huko Latin America. Lakini maendeleo kwa ujumla yamechanganyika.

“Bado kuna mwanya mkubwa baina ya matajiri na masikini, baina ya maeneo ya mashambani na mijini, baina ya wanaume na wanawake.” Alisema Bw. Ban Ki Moon.

Katibu mkuu alisema kwa kubuni mamilioni ya ajira duniani kote, na kuboresha afya ya mama na mtoto ni miongoni mwa mambo muhimu zaidi ambayo nchi zinaweza kutimiza katika malengo ya maendeleo ya millennia ya umoja mataifa.

Pia alitangaza kuanzishwa kwa kundi la uhamasishaji la MDG litakalo ongozwa na rais wa Rwanda Paul Kagame na waziri mkuu wa Uhispania Jose Luis Rodriguez Zapatero. Kundi hilo litajumlisha wataalam na wafadhili, ikiwa ni pamoja na washindi wa tuzo la Nobel, Waangari Maathai na Muhammed Yunus, na vilevile tajiri mwanzilishi wa kampuni ya Microsoft, Bill Gates. Bw. Ban alisema, jukumu lao litakuwa ni kushinikiza kuwepo kwa rai ya kisiasa na kuhamasisha makundi ya mashinani kufanikisha malengo yao ya maendeleo ya millennia. Mkutano wao wa kwanza utafanyika huko Uhispania mwezi ujao.

Hapo mwezi September Bw. Ban ataandaa mkutano wa siku 3 juu ya malengo ya maendeleo ya millennia, kabla ya mkutano wa baraza la umoja mataifa. Na baadaye wiki hii, Bw. Ban anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa G-20 huko Canada, ambapo anasema atawahimiza viongozi, wasitumie mzozo wa fedha duniani kama sababu ya kupunguza au kutotimiza ahadi zao za kutowa misaada.

XS
SM
MD
LG