Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Februari 25, 2024 Local time: 12:30

Maelfu waandamana kupinga ubakaji Kenya


Waandamanaji wakikabidhi barua katika ofisi ya inspekta mkuu wa Polisi nchini Kenya.
Waandamanaji wakikabidhi barua katika ofisi ya inspekta mkuu wa Polisi nchini Kenya.
Mamia ya waandamanaji waliingia mitaani jijini Nairobi Alhamis kudai haki kwa muathiriwa wa ubakaji ambaye wabakaji wake walipewa adhabu ya kufyeka nyasi na kisha kuachiwa.

Wakibeba mabango na baadhi ya wanawake wakibeba chupi zilizounganishwa pamoja kwa kamba walitoa ujumbe mkali wakikemea ghasia za ngono. Waandamanaji kote barani Afrika pia waliungana na wenzao wa Nairobi kuandamana kudai haki kwa msichana wa miaka 16 aliyebakwa huko Kenya.

Huko Nairobi maandamano yalianza katika bustani ya Uhuru park hadi kwenye mlango wa inspekta mkuu wa polisi, wakiwa na ujumbe mmoja uliokuwa kwenye maandishi ukisema “haki kwa Liz”.

Maandamano haya yaliandaliwa baada ya habari kuwa msichana huyo wa miaka 16 ambaye amepewa jina la utani “Liz na vyombo vya habari vya Kenya, alibakwa na genge la wanaume sita mwezi Juni alipokuwa akirudi nyumbani kwa mguu kutoka kwenye mazishi ya babu yake katika eneo la Busia magharibi mwa Kenya.

Msichana huyo aliumizwa sana katika shambulizi hilo na kisha kutupwa kwenye choo cha shimo. Baada ya kuokolewa kutoka chooni, hali yake ilibainika kuwa mbaya na sasa anatumia kigari cha gurudumu kwa sababu hawezi tena kutembea.

Wabakaji wake ambaye aliweza kuwatambua walipelekwa katika kituo kimoja cha polisi huko Busia ambapo walipewa adhabu ya kufyeka nyasi na kisha kuachiwa huru.

Waandamanaji hao waliwasilisha ombi lililotiwa saini na zaidi ya watu milioni moja kwenye mtandao kwa ofisi ya inspekta mkuu wa polisi David Kimaiyo. Ombi lao linataka wabakaji hao waadhibiwe na polisi walioipuuza kesi hiyo pia waadhibiwe.

Kesi ya kubakwa kwa msichana huyo iliandikwa kwanza na gazeti la Kenya ‘Daily Nation’ na kupata uungaji mkono wa haraka kutoka kwa makundi ya kutetea haki.

Emma Kaliya mwenyekiti wa kundi la maendeleo ya wanawake FEMNET anasema wanaharakati kutoka nchi 21 kote barani Afrika wameshiriki maandamano hayo ya Alhamis.

Maafisa wa Kenya akiwemo inspekta mkuu wa polisi bw. Kimaiyo wametoa hakikisho kuwa haki itatendwa.Naye mwendesha mashitaka wa serikali ameagiza kukamatwa kwa watuhumiwa hao sita lakini mpaka sasa hakuna aliyekamatwa.
XS
SM
MD
LG