Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Juni 09, 2023 Local time: 13:33

UN yamteua balozi wa Kenya kama mjumbe maalum kuhusu hali ya hewa


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, amemteua Balozi wa Kenya kwenye Umoja huo, Macharia Kamau, kama mjumbe maalum wa kushughulikia athari ziletwazo na hali ya hewa ya El Nino pamoja na maswala mengine yanayohusu mabadiliko ya hali ya hewa.

Na BMJ MURIITHI

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, amemteua Balozi wa Kenya katika Umoja huo, Macharia Kamau, kama mjumbe maalum wa kushughulikia athari ziletwazo na hali ya hewa ya El Nino pamoja na maswala mengine yanayohusu mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni kote.

Bw Kamau alipokea barua ya kumteua siku ya Ijumaa, tarehe 20 Mei, 2016, mjini New York. Moon aidha alimteua aliyekuwa rais wa Ireland Mary Robinson kwenye wadhifa huo.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na afisi ya Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa ilimtaja Kamau kama balozi mwenye uzoefu mwingi wa kidiplomasia.

"Ametumikia Umoja wa Mataifa kwa dhati," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa uteuzi huo umekuja wakati wa dharura kubwa ambapo dunia imeshuhudia ukame na mafuriko yanayohusiana na El Nino hasa Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika, Amerika ya Kati na Pasifiki.

Bwana Ban amesema Balozi Kamau na Bi Robinson watatoa uongozi unaohitajika kukabiliana na changamoto hizo pamoja na kutoa tahadhari inapobidi.

Na akizungumza na Sauti ya Amerika siku ya Jumamaosi, Bw Kamau aliutaja uteuzi huo kama ishara mwafaka kutoka kwa uongozi wa Shirika hilo.

"Ni fahari kubwa kwangu kuteuliwa kwenye wadhifa huu," alisema Kamau.

Aliahidi kufanya kila juhudi kuhakikisha kwamba changamoto za hali ya hewa zinazokumba mataifa yanayoendelea zimeangaziwa na vyombo husika kwenye shirika hilo.

"Nitayashinikiza mataifa yote, hususan yale yenye utajiri mkubwa duniani, kuwajibika hata zaidi ili kupunguza athari zinazoletwa na shughuli za binadamu kama vile wingi wa gesi chafu itokanayo na viwanda vikubwa vikubwa," alisema.

"Bara la Afrika limeathirika mno na vitendo vya mataifa tajiri," aliongeza balozi huyo bila kufafanua.

XS
SM
MD
LG