Mabalozi 11 wa nchi za magharibi mjini Nairobi walitoa onyo kali kwa mawaziri na maafisa wakuu wa serikali wanaohusika na rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma nchini Kenya kwamba huenda wakanyimwa vibali vya kuingia mataifa hayo ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa akaunti zao za benki katika mataifa hayo.
Wakiongea na wandishi wa habari baada ya kukutana na tume ya kupambana na rushwa mjini Nairobi, mabalozi hao wa nchi za magharibi walisema huenda serikali zao zikawanyima maafisa wa serikali vibali na hati za kuwaruhusu kuingia maataifa hayo ikiwa watapatikana na hatia ya wizi wa fedha za umma. Wakiongozwa na balozi wa Marekani mjini Nairobi, Bob Godec, mabalozi hao walisema wale watakao-patikana na hatia lazima wafikishwa mahakamani na kufungwa bila kujali cheo au utajiri walionao.
Baadhi ya mataifa ya magharibi yaliyotoa onyo hilo ni pamoja na Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Canada na Japan.
Lakini mapema Ijumaa kundi kubwa la wanawake kutoka jimbo la Embu, lililopo mashariki mwa Kenya liliandamana kupinga madai ya rushwa yanayotolewa dhidi yawaziri wa Ugatuzi bibi. Anne Waiguru.
Raia wa kawaida kutoka maeneo mbali mbali nchini Kenya wanazidi kulalamika kuhusu ongezeko kubwa la visa vya rushwa nchini Kenya.Wakuu wa kanisa la Anglicana, hapo Ijumaa walitoa taarifa kali ya kulaani tatizo la rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma kwenye serikali.