Wataalam wa mambo ya kale nchini Misri wamechimbua sehemu ya mabaki sanamu ya zaidi ya miaka elfu tatu ya mfalme wa zamani ambaye inaaminika alikuwa babu wa mfalme maarufu, Tut (Tutankhamun).
Mkuu wa maswala ya kale Misri, Zahi Hawass, anasema sanamu ya Amenhotep III (wa tatu) iligundulika mahali palipokuwa na makazi yake katika mji wa kusini wa Luxor. Hawass alisema Jumamosi mabaki hayo yanaonyesha Amenhotep akiwa amekaa katika kiti cha ufalme.
Wataalam wanaamini sanamu kamili ilikuwa na ukubwa wa karibu mita tatu.
Farao Amenhotep III alitawala ufalme wa Misri wakati wa kilele cha ustaarabu kutoka miaka ya 1390 hadi 1350 BC. Ufalme huo ulikuwa umeenea kutoka kaskazini ya Sudan ya sasa mpaka Syria.
Mjukuu wake, Mfalme Tut, alivutia macho ya dunia nzima baada ya wataalam kugundua kaburi lake likiwa limejaa vito vya thamani mwaka 1922. Mfalme huyo kijana wa chini ya miaka 20 alifariki 1324 BC.