Makabiliano yalizuka pia Jumanne katika maandamano kama hayo katika miji mingine ikiwemo Rennes, Bordeaux na Toulouse, huku tawi la benki na magari yakiteketezwa kwa moto katika mji wa Nantes.
Mapema mchana, serikali ilitupilia mbali ombi la vyama vya wafanyakazi la kusitisha na kufikiria upya mswaada huo wa pensheni, ambao unaongeza umri wa kustaafu kwa miaka miwili hadi miaka 64, na kuwakasirisha viongozi wa vyama vya wafanyakazi, ambao wamesema lazima serikali itafute njia ya kumaliza mzozo huo.
Serikali imesema iko tayari kuzungumza na vyama vya wafanyakazi kwa nia njema, lakini kuhusu mada nyingine, na imeeleza kwa mara nyingine kuwa itasimama kidete kuhusu masuala ya pensheni. Waziri mkuu Elisabeth Borne amekubali kukutana na vyama vya wafanyakazi Jumatatu na Jumanne wiki ijayo.