Kwa mjibu wa shirika la habari la AP, ilikuwa ni mapema nyakati za asubuhi ya Alhamisi wiki iliyopita, wakati wakazi katika kijiji kwenye jimbo la Yatenga waliamka na kuona kundi kubwa la watu waliokuwa na silaha waliovalia sare za kijeshi wakiendesha piki piki na magari yenye silaha, baadhi ya wanavijiji walitoka kwenye nyumba zao wakiwa na furaha kuwaona wanajeshi hao na kuwakaribisha.
Lakini kwa bahati mbaya furaha yao ilikatizwa wakati waliposikia milio ya risasi, na kusababisha vifo vya kwanza, ilisema taarifa kutoka kwa wana vijiji. Kamishna wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Ravina Shamdasani katika taarifa yake Jumanne amesema takriban wakazi 150 waliuwawa, huku wengine wengi wakijeruhiwa wakati wa shambulizi hilo.
Mapema wiki hii, ofisi ya mwendesha mashtaka ya Burkina Faso ilisema kwamba imeanzisha uchunguzi kuhusiana na mauaji hayo, ikisema kwamba idadi ya waliokufa ni 60, ikiwa chini ya nusu ya ile iliyoripotiwa na wakazi pamoja na UN.Kulingana na makundi ya kutetea haki za binadamu, mauaji kutoka kwa maafisa wa usalama yameongezeka Burkina Faso tangu Kapteni Ibrahim Traore alipochukua madaraka kupitia mapinduzi ya pili ya kijeshi Septemba 2022.
Mapema mwezi huu, serikali ya Burkina Faso ilitangaza kwamba ingeanza uchunguzi wa madai ya ukikukwaji wa haki za binadamu, uliofanywa na maafisa wake wa usalama, baada ya video kwenye mitandao kuonyesha watoto 7 wakiuwawa na maafisa, kaskazini mwa nchi.