Maafisa wa Ukraine Jumatano waliishutumu Russia baada ya video kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikidaiwa kumuonyesha mtu aliyevalia sare za kijeshi akimkata kichwa mtu ambaye mavazi yake ni pamoja na alama inayovaliwa na wanajeshi wa Ukraine.
Mashirika ya habari hayakuweza kuthibitisha mara moja ukweli wa video hiyo. Kuna kitu ambacho hakuna mtu duniani anayeweza kupuuza, jinsi wanyama hawa wanavyoua kwa urahisi, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alisema katika ujumbe wa video aliotuma Jumatano.
Zelenskyy alisema video hiyo inaonyesha kunyongwa kwa mateka wa Ukraine na kwamba kwa tukio hilo kila mtu lazima ajibu. Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov aliwaambia waandishi wa habari Jumatano kwamba video hiyo ni mbaya na kwamba ukweli wake unahitaji kuthibitishwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba, alirudia kueleza ukosoaji mpya wa Russia kushikilia urais wa kupokezana katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema Russia lazima ifukuzwe Ukraine na Umoja wa Mataifa na pia iwajibishwe kwa uhalifu wao.