Maafisa wa Marekani na Umoja wa Ulaya wameiambia Kosovo siku ya Jumatano kupunguza mvutano mkubwa na Wa-serbia, kaskazini mwa nchi hiyo au wakabiliane na adhabu kutoka kwa washirika wake wa muda mrefu wa Magharibi.
Onyo hilo limetolewa wakati wajumbe wa Marekani na Umoja wa Ulaya wakihitimisha ziara zao Kosovo na Serbia kutuliza mvutano uliozuka wiki iliyopita uliopelekea kujeruhiwa wanajeshi kadhaa wa kulinda amani wa NATO na waandamanaji wa Serbia huko kaskazini mwa Kosovo. Ghasia hizo zilizuka baada ya maafisa wa Kosovo kuwaweka kwa nguvu mameya wenye asili ya ki- Albania katika ofisi za manispaa.
Mameya walichaguliwa na asilimia 3.5 tu ya wapiga kura baada ya Wa-serbia, ambao ni wengi katika jimbo hilo kususia uchaguzi wa halmashauri za mitaa. Mjumbe wa Marekani katika kanda ya Balkani Magharibi, Gabriel Escobar amesema Kosovo lazima itoe uhuru mkubwa kwa manispaa zenye idadi kubwa ya watu wa Serbia ikiwa inataka kusogea karibu na kujiunga na NATO na Umoja wa Ulaya.
Hatua zilizochukuliwa au kutochukuliwa zinaweza kuwa na matokeo ambayo yataathiri sehemu za uhusiano kati ya Kosovo na Marekani. Sitaki kufika huko, Escobar aliviambia vyombo vya habari vya Kosovo siku ya Jumanne kabla ya kwenda Belgrade.
Forum