Maafisa wa Libya walirejea katika mji mkuu wa Misri leo Jumapili kwa ajili ya duru ya tatu ya mazungumzo kuhusu marekebisho ya katiba kwa ajili ya uchaguzi. Taifa hilo la Afrika Kaskazini kwa mara nyingine tena linajikuta katika mivutano ya kisiasa huku tawala mbili hasimu zikidai uhalali.
Mazungumzo hayo ya mjini Cairo yanakuja kufuatia mapigano kati ya wanamgambo hasimu yaliyosababisha wakazi wa mji mkuu wa Libya Tripoli kuingiwa na hofu na kufufua jinamizi la mapigano yaliyopita katika taifa hilo lililokumbwa na machafuko.
Wabunge kutoka bunge lenye makao yake mashariki mwa Libya na Baraza Kuu la nchi, chombo cha ushauri kutoka magharibi mwa Libya, walianza mazungumzo yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa huku kukiwa na shinikizo la kimataifa kwa mabunge hayo mawili kuweka mizozo yao kando na kukubaliana juu ya msingi wa kisheria wa uchaguzi.