Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 14:31

Mapambano yaendelea Tripoli


Wapiganaji wa upinzani nchini Libya wakiwa katika mji wa Tripoli, August 22, 2011
Wapiganaji wa upinzani nchini Libya wakiwa katika mji wa Tripoli, August 22, 2011

Mapambano kati ya majeshi yanayomtii kiongozi wa Libya Moammar Gadhafi na majeshi ya upinzani yanaendelea katika sehemu mbali mbali za mji mkuu, licha ya upinzani kudai kudhibiti eneo la Tripoli

Majeshi yanayomtii Moammar Gadhafi yamepambana na waasi katika sehemu kadhaa za mji mkuu wa Libya, Tripoli Jumatatu usiku, wakati mtoto wa kiume wa kiongozi huyo aliyetarajiwa wakati mmoja kuwa mrithi wake, Seif al-Islam, alikuwa akitemnbea kwa uhuru mjini Tripoli licha ya upinzani kudai walimkamata kijana huyo.

Seif al-Islam alienda mwenyewe kwa waandishi wa habari wa kigeni waliowekwa kwenye hoteli ya Rixos inayodhibitiwa na wafuasi wa Gadhafi mapema Jumanne. Amewaambia waandishi wa habari kwamba serikali ya baba yake bado inadhibiti Tripoli na iliwavutia waasi kuingia katika mtego kwa kuwaruhusu kuingia katika mji bila ya upinzani. Baada ya hapo aliongoza tena mlolongo wa magari kupita mitaa inayoshikiliwa na wafuasi wake ambako picha za televisheni zilionesha akishangiriwa na wafuasi wake.

Siku ya Jumapili viongozi wa upinzani pamoja na mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC ilisema kwamba Seif al-Islam, ambaye amefunguliwa mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu alikuwa akishikiliwa na waasi. Vyanzo kutoka upande wa waasi pia vilisema mtoto mwingine wa kiume wa bwana Gadhafi, Mohammed alikimbia kifungo cha nyumbani hapo Jumatatu. Mtoto mwingine wa tatu bado anashikiliwa.

Wakati huo huo mkuu wa baraza la mpito la kitaifa, Mustafa Abdel Jalil, alisema waasi hawajui kama kiongozi huyo wa Libya bado yupo nchini humo. Alisema bwana Gadhafi atafunguliwa kesi iliyo ya haki kama akikamatwa na kwamba wakati wa kweli wa ushindi utakuwa pale wakati atakapokamatwa.

Jalil alikiri kwamba waasi bado hawajaidhibiti kikamilifu Tripoli. Wapiganaji wa upinzani wanasema majeshi yanayoiunga mkono serikali bado wanashikilia asilimia 10 hadi 15 ya mji mkuu ikiwemo uwanja wa nyumba ya bwana Gadhafi wa Bab al-Aziziya.

Mapigano yalipamba moto mapema wakati vifaru vilipoonekana kutoka uwanja huo na kufyatua risasi licha ya miezi kadhaa ya mashambulizi ya anga ya NATO yaliyosababisha uharibifu mkubwa kwenye uwanja huo.

XS
SM
MD
LG