Chama cha mapinduzi na ustawi (RFP) ambacho kiliundwa miezi sita iliyopita na mfanyabiashara asiyekuwa na uzoefu wa kisiasa Sam Matekane, mwenye umri wa miaka 64, kilipata viti 56 kati ya 120, kulingana na matokeo ya mwisho yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi jana Jumatatu.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Matekane amesema RFP imeunda serikali ya mungano na chama cha Alliance of Democrats (AD) na Movement for Economic Change (MEC).
Chama cha AD kilipata viti sita katika uchaguzi huo uliofanyika siku ya Ijumaa, nacho chama cha MEC kilipata viti vitano.
Taifa hilo dogo la kifalme liliongozwa katika muongo mmoja uliopita na serikali kadhaa za muungano ambazo zilikumbwa na migawanyiko, na hakuna waziri mkuu aliyeongoza muhula kamili wa miaka mitano.