Mashindano ya kandanda ya nchi za Ulaya UEFA yanayoendelea nchini Ufaransa yanaonekana ni ya kusisimua na yanazidi kuwavutia maelfu ya washabiki wa soka duniani kote. Mashindano hayo ambayo sasa yanaelekea kwenye hatua za mtoano baada ya kushuhudia hatua za makundi zikifikia ukingoni, yametoa taswira mpya kabisa katika ulimwengu wa soka.
Gumzo kubwa kabisa ni kiwango cha soka kilichoonyeshwa na timu ya Hispania ambayo kutokana na kutofanya vizuri katika mashindano ya kombe la dunia yaliyopita, haikutarajiwa kuwa wangerudi na kucheza mpira wa hali ya juu sana waliouonyesha katika mashindano haya.
Ufaransa, wageni wa mashindano haya, wameonyesha ari kubwa na ufundi wa hali ya juu sana wa kusakata kabumbu na bado wana nafasi kubwa sana ya kulibakisha kombe hili mikononi mwao baada ya kufanikiwa kupita katika hatua ya makundi bila mikwaruzo, ingawa haitarajiwi kuwa rahisi kutokana na uwepo wa timu nzuri sana kama Ujerumani na Hispania.
Uingereza ni timu nyingine ambayo haijapewa nafasi sana na haijaweza kuonyesha kiwango bora zaidi lakini wameweza kupita kwenye hatua za makundi mpaka mtoano mapema zaidi. Bado inaonekana kuna kazi sana kuweza kuiweka uingereza katika kundi la washindi watarajiwa.
Croatia timu yenye viungo wenye vipaji vya hali ya juu wamegubikwa na tatizo la mashabiki wenye hasira na fujo. Tayari uefa wameipiga faini kubwa ya euro laki moja Croatia kwa fujo hizo zilizotokea St. Etienne wakati wa mchezo wao na timu ya Jamhuri ya Czech. Inasadikika kuwa mashabiki walifanya fujo kwa sababu ya kutokubaliana na chama cha soka cha Croatia na makamu wa rais wa chama hicho Zdravko Mamic.