Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Januari 18, 2025 Local time: 16:19

Kura zahesabiwa Algeria katika hatua ya kubadilisha katiba


Mpiga kura nchini Algeria
Mpiga kura nchini Algeria

Maafisa wa uchaguzi nchini Algeria wanaendelea na mchakato wa kuhesabu kura katika kura ya maoni kufanyia mabadiliko katiba ya nchi hiyo.

Maafisa wanaripoti idadi ndogo sana ya wapiga kura waliojitokeza kwa uchaguzi huo ambao lengo lake ni kuleta mabadiliko nchini humo kufuatia maandamano ya kisiasa mwaka uliopita.

Rais Abdelmadjid Tebboune na utawala wa kijeshi, wanataka katiba ya nchi hiyo kufanyiwa marekebisho huku viongozi wa maandamano makubwa ya mwaka uliopita wakiwa wamepinga kura hiyo wakiitaja kuwa ulaghai.

Maafisa wamesema kwamba asilimia 20 pekee ya wapiga kura wameshiriki zoezi hilo.

Asilimia 40 ya wapiga kura walijitokeza katika uchaguzi mkuu wa urais mwezi Desemba mwaka uliopita.

Tebboune, amelazwa hospitalini nchini Ujerumani tangu wiki iliyopita baada ya kusema kwamba baadhi ya maafisa walio karibu naye wameambukizwa virusi vya Corona.

Amekuwa akiwahimiza raia wa Algeria kujitokeza kwa wingi kupitisha mabadiliko ya katiba ya nchi hiyo ili kumaliza maandamano.

Vituo vya kupiga kura vimeshuhudia idadi ndogo sana ya wapiga kura katika maeneo mengi ya nchi.

Maandamano yametokea eneo la Kabyelie, waandamanaji wakifunga vituo vya kupigia kura.

“Hakuna haja ya kupiga kura. Katiba haitabadilisha kitu chochote.” Amesema Hassan Rabia, ambaye ni dereva katikati mwa Algiers.

Rais Tebboune ametaka wapiga kura nchini humo kubadilisha katiba akisema italeta mabadiliko makubwa ya uongozi na ukuaji wa uchumi nchini humo baada ya maandamano ya mwaka uliopota yaliyofikisha mwisho wa utawala wa miaka 20 wa Abdelaziz Bouteflika.

Waandamanaji wanataka jeshi kuachana kabisa na siasa, Pamoja na kutaka serikali kumaliza ufisadi, matakwa ambayo hayajatimizwa kabisa.

Katiba mpya inapendekeza kuwepo kikomo kwa mihula ya utawala wa rais, bunge na mahakama kupewa mamlaka zaidi.

Hata hivyo, jeshi linasalia kuwa na mamlaka makubwa sana katika siasa za nchi hiyo, japo halijakuwa na mchango mkubwa sana katika uongozi wa nchi hiyo tangu Tebboune alipoingia madarakani.

Katiba mpya inatoa mamlaka kwa jeshi kuingilia maswala ya usalama wa nchi zingine, huku magenerali wake wakiwa wanaelezea wasiwasi kuhusu hali ya usalama nchini Libya na Mali.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG