Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Machi 25, 2023 Local time: 17:49

Hesabu za kura Kenya zaendelea


Mgombea urais Bw. Uhuru Kenyatta akipiga kura katika shule ya Mutomo, eneo la Gatundu alikozaliwa Machi 4, 2013

Mkuu wa tume ya uchaguzi Isaack Hassan anasema hakuna matokeo zaidi ya ghasia yaliyoripotiwa tangu tukio la awali la kushambuliwa polisi huko Mombasa.

Uchaguzi mkuu wa Kenya umefanyika Jumatatu katika kile maafisa wa tume huru ya uchaguzi I.E.B.C. wanasema ulikuwa wa kihistoria. Kufikia saa mbili jioni saa za Kenya matokeo ya kura zilizohesabiwa yalionyesha mgombea urais Bw. Uhuru Kenyatta wa chama cha TNA na muungano Jubilee alikuwa anaongoza kwa asili mia 57 akifuatiwa na Bw. Raila Odinga wa chama cha ODM na muungano wa Cord kwa asili mia 38 ya kura zilizohesabiwa. Lakini hiyo ni awali mno bado kuna kura nyingi hazijahesabiwa.

Wakenya wengi walijitokeza tangu saa tisa alfajiri kupanga foleni kwenye vituo mbalimbali vya kupigia kura. Bw. Kenyatta alipiga kura yake saa tano na robo mchana kwa saa kwa Kenya katika shule ya Mutomo katika eneo la Gatundu anakotoka, na kuwasihi Wakenya kuwa watulivu na kujiepusha na ghasia wanaposubiri matokeo ya uchaguzi huo akisema ana matumaini makuu kushinda kiti cha urais.

Naye mgombea urais bwana Raila Odinga wa chama cha ODM na Muungano wa Cord alipigia kura yake katika shule ya msingi ya Old Kibera, iliyoko eneo bunge la Kibra nje kidogo ya mji wa Nairobi. Bwana Odinga aliitaka serikali kuongeza ulinzi kwenye vituo vya kupigia kura na pia kutoa mwito wa amani.

Akizungumza na sauti ya Amerika, kamishina wa tume huru ya uchaguzi I.E.B.C Balozi Yusuf Nzibo alisema kulitokea mauaji ya watu kadhaa katika eneo la Mombasa akiwemo afisa mmoja wa tume hiyo. Alisema licha ya matatizo madogo ya hapa na pale uchaguzi huo umekwenda vizuri. Kura zimeanza kuhesabiwa na tume hiyo ya uchaguzi inakisia kuwa itaweza kuwa na matokeo rasmi ya mshindi wa kiti cha urais ifikapo saa sita mchana Jumanne.
XS
SM
MD
LG