Majuma mawili yaliopita, Umar Mohammed alikamata mshukiwa kutoka kundi la Boko Haram aliekuwa akijaribu kuingia kwenye mji wa kaskazini mashariki wa Maiduguri akiwa amebeba bomu.
Mohammed ni mmoja kutoka kikosi maalum cha kiraiya maarufu 'Civilian Joint Task Force' (JTF) ambacho kimeidhinishwa na serikali ya jimbo la Borno tangu mwaka wa 2013 kwa lengo la kukabiliana na Boko Haram.
Kundi la Boko Haram limekuwa likifanya mashambulizi kaskazini mashariki mwa Nigeria na pia kwenye eneo la ziwa Chad kwa miaka saba huku likiuwa zaidi ya watu 20,000 na kusababisha wengine milioni 2.7 kukosa makao.
Operesheni ya kijeshi kwenye eneo hilo imemaliza nguvu za Boko Haram na hata kuliondoa kwenye maeneo ya mjini.
Makundi kama vile 'JTF' pamoja na mengine takriban darzeni moja kwenye eneo hilo pia yamesaidia pakubwa katika kuangamiza kundi hilo.