Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 19:17

Kumbukumbu ya Dr. Martin Luther King Jr.


Dr. Martin Luther King Jr. akitoa hotuba Aug 28,1963
Dr. Martin Luther King Jr. akitoa hotuba Aug 28,1963
Miaka hamsini iliyopita Mchungaji Martin Luther King Junior aliongoza maandamano yaliyobadilisha maisha ya wamarekani wote. Mnamo Agosti 28 mwaka wa 1963, King alitoa hotuba yake maarufu ‘ I Have a Dream” kwa umati mkubwa wa zaidi ya watu laki mbili na nusu hapa Washington. Tukio hilo lilibadilika kuwa la kihistoria nchini Marekani.

Watu robo milioni waliandamana kutetea haki sawa na ajira. Maandamano hayo yalifanyika wakati wa ghasia kubwa za ubaguzi wa rangi huku Marekani ikitafuta ufumbuzi wa sheria zake zilizobagua wamarekani weusi wenye asili ya Kiafrika. Mchungaji Jesse Jackson anasema Martin Luther King alikuwa na maono sahihi juu ya maandamano hayo ya kihistoria.

Waliohudhuria mkusanyiko huo wanasema ulikuwa wa kisherehe. Wasomi wengi wa historia wanakubaliana kuwa maandamano hayo yalitoa ujumbe mzito kwamba sharti ubaguzi wa rangi ufike kikomo. Mchungaji Willie Blue anasema hakutegemea tukio hilo lingekuwa la uzito ule.

Dr. King alitumia mkusanyiko huo mkubwa wa watu kutoa hotuba yake maarufu, I have a dream akieleza kuwa ana ndoto, kwamba watu wote duniani waliumbwa sawa.Aliashiria shida za Wamarekani weusi wakijaribu kupigana dhidi ya ubaguzi wa rangi. Lakini kilele cha hotuba ya Dr. King kilikuwa pale alipoelezea kuhusu maazimio binafsi ya taifa la Marekani.
‘Nina ndoto kuwa wanangu wanne siku moja wataishi katika taifa ambalo maamuzi juu yao hayatafanywa kwa misingi ya rangi yao, lakini kwa matendo ya tabia zao. Nina ndoto leo”

Mbunge wa Marekani John Lewis ambaye alizungumza wakati wa maandamano hayo, anasema matamshi ya Dr. King yanasisimua. Alisema “Alibadili ngazi zinazoelekea kwenye mnara wa kumbukumbu wa Lincoln kuwa kama eneo la mchungaji anapohubiri na namkumbuka akisema nitaota leo, ndoto inayokita mizizi yake kwenye ndoto za Marekani.”

Naye Dick Miles alikuwa miongoni mwa wazungu wengi walioshiriki maandamano hayo.alisema hakudhani kuna mmoja wao aliyetegemea hotuba ya kusisimua kama waliyoisikia. ‘Iligusa kila mmoja moyoni.”
Maandamno ya Washington yalimalizika Dr. King akiwaomba wamarekani wote wakubali uhuru utawale.

Mbunge John Lewis anakumbuka kuwa watu walipoanza kurejea makwao, viongozi wa haki za kiraia walikutana White House na rais John Kennedy ambaye aliwaalika White House. Lewis alimwelezea rais Kennedy kama baba aliyefurahia vitendo vya wanawe; ‘alitwambia kila mmoja, ‘mmefanya kazi nzuri, na alipomfikia Dr. King, akasema ‘na wewe ulikuwa na ndoto.”

King alisema maandamano hayo yatakuwa mojawapo ya maandamano makubwa katika historia ya kutetea uhuru na hadhi ya binadamu kuwahi kufanyika Marekani. Wasomi wa historia wanasema maandamano hayo ya Washington yalikuwa ya amani na bila shaka yoyote yalibadilisha taifa la Marekani.
XS
SM
MD
LG