Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye amekamatwa tena leo - mara ya tatu katika muda wa wiki mbili - akiwa njiani kwenda kazini kwa miguu, hatua ambayo serikali inasema ni njama za kufanya maandamano yasiyo halali.
Besigye na wafuasi wake wamekuwa wakitembea kwa miguu kwenda kazini kila Jumatatu na Alhamisi kupinga ongezeko la bei za mafuta na chakula nchini humo pamoja na matumizi mabaya ya mali ya umma wanayodai kufanywa na serikali ya rais Museveni.
Lakini serikali inasema matembezi hayo ni maandamano yasiyo halali na kwamba itawakamata ambao wanashiriki katika maandamano hayo.
Ripoti nyingine kutoka Kampala zinasema leo kuwa Besigye ameondolewa mjini Kampala na anashikiliwa sehemu nyingine ndani ya nchi hiyo ili kuondoa uwezekano wa wafuasi wake kufanya fujo mjini Kampala