Upatikanaji viungo

Kiongozi wa waasi wa M23 azungumza na VOA

  • Esther Githui-Ewart
  • Mkamiti Kibayasi

Kiongozi wa M23, Jean-Marie Runiga akishuka kwenye gari ili kuzungumza na vyombo vya habari mjini Goma, DRC, November 27, 2012.
Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika-VOA Ijumaa katika mahojiano ya moja kwa moja kiongozi wa kundi la uasi la M23, Jean Marie Runiga alisema yeye ni mtumishi wa Mungu na kwamba ni askofu aliyeamua kuunda kundi la waasi ili ‘kutetea haki za wanyonge’ katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.


Bw. Runiga amesema Mungu hapendi kuona binadamu wakitaabika na hivyo aliona kheri kuanza juhudi kuwakomboa wakongomani ambao hawajui maisha mengine ila taabu na mateso. Kiongozi huyo wa M23 amesema serikali ya Kabila imeshindwa kuwahudumia raia wa Congo na kwamba wengi wanakufa kila siku sio kwa sababu ya vita bali ukosefu wa huduma za kimsingi kama vile chakula na matibabu.

Alisema DRC haina miundombinu, haina barabara, haina hospitali , wala shule za kutegemewa. Alisema wanawake wanazidi kubakwa yote haya akilaumu uongozi anaosema si halali wa serikali ya Rais Joseph Kabila. Bw. Runiga amesema mwishoni mwa wiki hii kundi lake na wawakilishi wa serikali ya DRC wanakutana Kampala, Uganda kuendela na juhudi mazungumzo ya kutafuta amani nchini Congo. Alisisitiza kuwa kundi lake linatoa nafasi ya amani kwanza, kwa ajili ya raia wa Congo.

Pia alikanusha madai kuwa Rwanda inafadhili kundi hilo akiongeza kwamba M23 halijapewa msaada wowote kutoka nje.

Maoni yako

Onyesha maoni

XS
SM
MD
LG