Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Novemba 08, 2024 Local time: 23:32

Kiongozi wa juu wa Iran aahidi ulipizaji kisasi wa mauaji ya mwanasayansi 


Hayati Mohsen Fakhrizadeh
Hayati Mohsen Fakhrizadeh

Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Jumamosi ametoa amri ya “adhabu itolewe” kwa wale waliohusika na mauaji ya mwanasayansi anayehusishwa na programu ya nyuklia ya kijeshi, mauaji ambayo Jamhuri ya Kiislam imeilaumu Israeli.

Israeli, kwa muda mrefu ikishukiwa kuhusika na mauaji ya wanasayansi wa Iran muongo moja uliopita wakati mivutano ikiendelea juu ya program ya nyuklia ya Tehran, haijatoa tamko lolote la mauaji ya Mohsen Fakhrizadeh yaliofanyika Ijumaa. Hata hivyo shambulizi hilo linaonyesha dalili zote za mipango makini, kwa staili ya uvamizi wa kijeshi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP mauaji hayo yanatishia kuibua tena mgogoro kati ya Marekani na Iran katika siku za mwisho za utawala wa Rais Donald Trump, wakati Rais mteule Joe Biden amependekeza utawala wake ungeweza kurejea katika mkataba wa nyuklia wa Tehran uliosainiwa na nchi zenye nguvu duniani ambao mapema Trump alijiondoa.

Wizara ya Ulinzi ya Marekani imetangaza mapema Jumamosi kuwa inapeleka manuari ya Marekani USS Nimitz inayobeba ndege za kivita huko Mashariki ya Kati.

Katika tamko lake, Kiongozi mkuu Ayatollah Ali Khamenei amemtaja Fakhrizdeh kuwa ni “mwanasayansi mashuhuri na wakipekee wa vifaa vya nyuklia na ulinzi.”

Khamenei amesema kipaumbele cha kwanza cha Iran baada ya mauaji hayo ni “uamuzi wa kuwaadhibu waliofanya uovu huo na wale walioamrisha.” Lakini hakufafanua zaidi.

Akizungumza katika mkutano wa kikosi kazi cha serikali cha kupambana na virusi vya corona Jumamosi, Rais Hassan Rouhani ameilaumu Israeli kwa mauaji hayo.

Rouhani amesema kuwa kifo cha Fakhrizadeh hakitazuia programu ya nyuklia kuendelea, kitu ambacho amesema pia Khamenei. Programu ya matumizi ya kawaida ya nyuklia imeendelea na majaribio yake na hivi sasa inarutubisha uranium kwa asilimia 4.5 chini ya kiwango kinachotengeneza silaha cha asilimia 90.

Lakini wachambuzi wanamlinganisha Fakhrizadeh kuwa sawa na Robert Oppenheimer, mwanasayansi aliyeongoza Mradi wa Manhattan ya Vita vya Pili vya Dunia uliotengeneza bomu la atomic.

“Tutajibu shambulizi hili la mauaji ya Fakhrizadeh katika wakati unaostahili,” amesema Rouhani.

Ameongoza kuwa: Taifa la Iran ni mahiri zaidi haliwezi kutumbukia katika mtego wa Wazayuni. Wanafikiria kuleta machafuko.”

Shambulizi la Ijumaa lilitokea Absard, kijiji mashariki ya mji mkuu ambacho ni mapumziko ya wasomi wa Iran. Televisheni ya Taifa ya Iran imesema gari chakavu lililokuwa na vilipuzi lililokuwa limefichwa chini ya mzigo wa mbao uliripuka karibu na gari ndogo iliyokuwa imembeba Fakhrizadeh.

Wakati gari ya Fakhrizadeh iliposimama, watu wasiopungua watano wenye bunduki walitokea na kuichakaza gari hiyo kwa risasi zenye nguvu, Shirika la habari la Tasnim limesema.

Fakhrizadeh alifariki hospitalini baada ya madaktari na wauguzi kushindwa kumwezesha kupumua. Wengine waliojeruhiwa ni pamoja na walinzi wa Fakhrizadeh.

Saa kadhaa baada ya shambulizi hilo, Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilitangaza imerejesha manuari inayobeba ndege za kivita USS Nimitz Mashariki ya Kati, kitendo ambacho si cha kawaida kwani manuari hiyo ilikuwa imekaa kwa miezi kadhaa katika eneo hilo.

Ilieleza kuwa kuondolewa kwa vikosi vya Marekani nchini Afghanistan na Iraq kuwa ni sababu ya kuleta manuari hiyo, ikisema “ ilikuwa busara kuongeza ulinzi wa ziada katika eneo ili kukabiliana na chochote kitakacho tokea.”

Shambulizi hili limetokea siku chache kabla ya maadhimisho ya miaka 10 ya mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran Majid Shahriari ambalo Tehran iliilaumu Israeli.

XS
SM
MD
LG