Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Septemba 21, 2024 Local time: 06:54

Wafuasi wa Chadema washeherekea kuachiwa huru kwa Freeman Mbowe


Freeman Mbowe kiongozi wa CHADEMA alpozungumza na waandishi habari
Freeman Mbowe kiongozi wa CHADEMA alpozungumza na waandishi habari

Mahakama ya Tanzania Ijumaa ilitupilia mbali mashtaka ya ugaidi dhidi ya kiongozi wa upinzani Freeman Mbowe na kuamuru aachiliwe huru mara moja.

Wafuasi wa chama cha upinzani cha Chadema nchini Tanzania walishanglia kwa nderemo na vifijo mahakamani na kufanya maombi ya shukrani baada ya kiongozi wao Freeman Mbowe kuachiliwa huru kutokana na kesi ya ugaidi iliyokuwa ikimkabili.

Mbowe pamoja na wenzake wengine watatu wameachiwa huru baada ya Jamhuri kuwasilisha taarifa mahakamani kusudio la kutotaka kuendelea na kesi hiyo.

Kiongozi huyo wa upinzani ambaye yeye pamoja na wenzake ilikuwa leo waanze kutoa ushahidi wao, alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya ugaidi pamoja na uhujumu uchumi makosa ambayo hayana dhamana.

Yeye alikamatwa kwa mara ya kwanza jijini Mwanza wakati akiwa kwenye kampeni ya kuendesha mikutano ya ndani iliyokuwa na lengo la kuhamasisha umma kuhusu madai ya katiba mpya

Kumekuwa na hali ya shangwe kutoka kwa wafuasi wa chama hicho kufuatia hatua ya makama kuu diviseni ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi kumwachia huru kiongozi huyo.

Wafuasi wa chama hicho waliofurika kwa wingi mahakamani hapo, mbali ya kuonyesha hisia za furaha lakini wamekosoa namna kiongozi wao alivyotumbukia kwenye kesi hiyo.

Mmoja wa mawakili wa Mbowe, Peter Kibatala amesema mteja wake amepitia madhila mengi lakini jambo la kufurahisha ameachiwa huru.

Ameitaja kesi ya Mbowe kuwa ni moja ya mashauri magumu aliyowahi kupitia kutokana na namna ilivyogusa maslahi ya wengi.

Tangu kutiwa kwake mbaroni hadi dakika hii kumekuwa na wito wa kutaka kesi hiyo ifutwe wakidai mashtaka dhidi yake yalishinikizwa kisiasa.

Mbowe hajazungumza lolote makahamani hapo, lakini wakili wake amesema huenda akafanya hivyo katika siku za baadaye. “ Kwa sasa tumemshauri Mbowe apumzike kwanza na asizungumze lolote maana mtu ukitoka katika hali hii halafu azungumze unaweza kutoa matamshi yenye hisia na kuzua jambo lingine… atazungumza katika siku za usoni,” alisema.

Shinikizo la kutaka Mbowe aachiwe huru lilipata nguvu mpya katika siku za hivi karibuni na mapema mwezi uliopita, makamu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alikutana na Rais Samia Suluhu Hassan na kumtaka kutumia busara zake katika kushughulikia kesi hiyo.

Walipokutana na Rais Ikulu Dar es salaam jana, viongozi wa dini pamoja na mambo mengine waliyojadiliana naye lakini pia suala la Mbowe lilijitokeza wakisihi kuwepo kwa busara katika kushughulikia kesi dhidi ya kiongozi huyo.

Kesi ya Mbowe ilikuwa ni moja ya ajenda iliyoteka karibu maeneo yote ya nchi na kwingineko duniani huku pia wanadiplomasia wa nchi za magharibi wakifika wakati wote mahakani hapo kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo.

XS
SM
MD
LG