Kufuatia mjadala mkali bungeni kuhusu matumizi mabaya ya fedha na juhudi za kutaka kuwasilisha hoja ya kutokua na imani na Waziri Mkuu, Rais Kikwete ameiarifu kamati kuu ya chama tawala cha CCM katika kikao cha dharura kwamba atafanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye ameiambia Sauti ya Amarika kwamba, "kamati kuu imepokea kwa furaha na kwa kweli imeridhia na kubariki uwamuzi wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kulisuka upya baraza la mawaziri, na kuwawajibisha mawaziri kwa mujibu wa jinsi walivyohusika na kuhusishwa kwenye zile taarifa."
Bw. Nnauye alisema mbali na kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri atawawajibisha watendaji wa serikali na baadhi ya mashirika ya umma, ambao wamehusishwa kwenye hizo taarifa.
Msemaji wa Ikulu Salva Rweyemamu amethibitisha uwamuzi huo alipozungumza na Sauti ya Amerika akisema Rais mwenyewe ndiye aliyeliagizia bunge kujadili kwa kina ripoti zote za kamati ya mahesebu ya serikali kwa sababu hiyo ndio kazi ya bunge.
Anasema kufutia matokeo ya ripoti na mapendekezo ya wabunge Rais hana budi ila kuchukua hatua kulingana na jinsi anavyo ona yeye binafsi.
Bw.Rweyemamu anasema hajui lini Rais Kikwete ataamua kufanyamabadiliko ya baraza la mawaziri lakini haitachukua muda mrefu kabla ya yeye kuwaarifu wananchi juu ya uwamuzi wake.