Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Juni 07, 2023 Local time: 02:14

Kifo cha Mwandishi Tanzania: Polisi watakiwa kuwajibika


Ramani ya Tanzania

Waandishi wataka uongozi wa jeshi la polisi Tanzania kuwajibika kuanzia kamanda wa polisi wa mkoa na uongozi wa makao makuu akiwamo -IGP, Saidi Mwema.

Viongozi wa vyama vya siasa, wanaharakati, waandishi wa habari na wananchi wa kawaida jijini Dar es salaam, wamezungumzia tukio la kuuwawa kwa mwandishi mmoja wa habari Daudi Mwangosi katika vurugu zilizotokea jumapili mkoani Iringa zilizohusisha
jeshi la polisi na wafuasi wa chama cha upinzani cha CHADEMA

Watu wengi waliohojiwa kuhusu kifo cha mwandishi huyo walidai kuwa mauaji hayo yametokana na polisi kutumia nguvu kupita kiasi, huku wakitaka tume huru iundwe ili kufanya uchunguzi wa kina wa chanzo kilichopelekea kifo cha mwandishi huyo.

Wakati huo huo jukwaa la wahariri kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania, wameunda timu ya uchunguzi wa suala hilo ambayo itakwenda mkoani Iringa ili kubaini ukweli wa tukio hilo. Lengo la uchunguzi huo ni kuweka kumbukumbu sahihi ya tukio hilo.

Katika tamko lake Jumatatu, jukwaa hilo la wahariri limesema tukio la mauaji ya mwandishi wa habari linaiingiza Tanzania katika historia mbaya ya ukiukwaji na ukandamizwaji wa uhuru wa habari, kwani ni kwa mara ya kwanza nchi inashuhudia mwandishi wa habari akiuwawa wakati akitekeleza majukumu ya kazi yake

Naye kaimu katibu mkuu wa chama cha UDP, Isaac Cheyo ametaka jeshi la polisi kuacha kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa kutuliza ghasia. Amawataka polisi kuacha kutumika jeshi hilo kama chombo cha kuweka mbele maslahi ya watawala badala ya umma wa watanzania.

Pia mwenyekiti wa chama cha siasa cha NLD Dk.Emmanuel Makaidi, ametaka kuwepo kwa chombo huru cha kuchunguza matukio yanayohusisha jeshi la polisi kuliko ilivyo hivi sasa, jeshi kuunda timu ya uchunguzi kujichunguza yenyewe.

Daudi Mwangosi licha ya kuwa mwakilishi wa kituo cha televisheni cha channel Ten cha jijini Dar es salaam alikuwa mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoani Iringa.

Waandishi wametaka uongozi wa jeshi la polisi nchini Tanzania kuwajibika kuanzia kamanda wa polisi wa mkoa na uongozi wa makao makuu, akiwamo Mkuu wa Jeshi la Polisi -IGP, Saidi Mwema.

Mwandishi huyo wa habari anatarajiwa kuzikwa jumanne Tukuyu Mkoani Mbeya.
XS
SM
MD
LG