Kenya inapambana na wimbi la maambukizi makubwa ya Covid 19 kuwahi kutokea tangu kuzuka kwa janga la virusi vya corona mwaka 2020.
Idadi ya watu wanaogundulika kuwa na virusi vya corona imepanda kutoka asilimia 6.5 hadi 30 katika wiki moja iliyopita.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeitaja nchi hiyo kuwa iko katika hatari zaidi kutokana na viwango vya wale wanagundulika wamepata maambukizi ikiwa ni zaidi ya asilimia 5 na kuzishauri nchi zilizoathiriwa kufikiria kuweka masharti ili kupunguza kuenea kwa virusi hivyo.
Hata hivyo, mkuu wa kundi la utafiti katika Amref Health Africa International, Githinji Gitahi anasema kwamba watu wengi wanakwenda hospitali kupata msaada wa matibabu ya virusi vya corona na hawana haja ya kulazwa hospitali.
“Tuna Wagonjwa wengi ambao wanafika tu kliniki, katika mahospitali lakini kwa kiasi ni wagonjwa wanaotibiwa na kuondoka, idadi ya wagonjwa hao imeongezeka maradufu lakini siyo wanaolazwa hospitali. Hatuoni wagonjwa wengi wakilazwa hospitali, wakihitaji mashine ya kuwasaidia kupumua, kuwekwa katika vyumba vya watu mahututi ICU-HDU kama ilivyokuwa ikitarajiwa hapo kabla, ambapo inaashiria kwamba huenda kinga katika miili yao waliyokuwa nayo inapambana na maambukizi, chanjo ya mapema au virusi si vikali sana na kusababisha mtu kuugua,” anasema Gitahi.
Baadhi ya nchi zimeanzisha tena masharti ya kufunga shughuli ili kupambana na kusambaa kwa Omicron. Lakini taifa hilo la Afrika Mashariki limekuwa likisita kufanya hivyo.
Dr. David Sang, mtaalamu wa magonjwa ya mlipuko, anasema watu wameonyesha kujiachia kidogo katika baadhi ya kanuni za kiafya kama kuvaa barakoa na kuosha mikono kila mara.
Nchini Kenya, kuvaa barakoa ni lazima, lakini siku hizi amri hiyo ni nadra sana kufuatwa au kutekelezwa.
Gitahi anasema nchi itaendelea kuwa na mawimbi ya Covid 19 mpaka wananchi wengi zaidi wawe wamepatiwa chanjo.
Katika ya takriban watu milioni 54 nchini Kenya, kiasi cha milioni 9 wamepatiwa walau dozi moja ya chanjo ya Covid 19, na 3.6 millioni ndiyo wamepata chanjo kamili.