Zaidi ya wajumbe 300 kutoka mataifa 22 katika bara la Afrika na takribani mashirika 16 yanayohusika na masuala ya usalama duniani wanakutana mjini Nairobi, Kenya katika kongamano la kujadili mikakati mipya ya kupambana na visa vya kigaidi katika bara la Afrika na ulimwengu kwa jumla.
Waziri wa Ulinzi wa Kenya, Joseph Ngaisari ambaye ndio mwenyeji wa mkutano huo anashirikiana na washiriki kwenye kongamano hilo juu ya kukabiliana na visa vya kigaidi. “naalika mataifa mengine ya Afrika 22 na nchi nyingine 16 sio kutoka ndani ya bara la Afrika tu, wale wanaohusika na mambo ya ugaidi na ndipo tukasema tuje tujadiliane tutafute mbinu za kuweza kupigana na huyu adui hasa wale wanaowashawishi vijana wetu mambo ya ugaidi”.
Baadhi ya mataifa ya bara la Afrika yaliyoathirika zaidi na visa vya kigaidi ni Kenya na Nigeria. Kenya imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara na magaidi wa kundi la al-Shabab lenye makao yake nchini Somalia. Kundi la al-Shabab lilifanya shambulizi kubwa hivi karibuni katika chuo kikuu cha Garissa na kuwauwa watu wasiopungua 150, wengi wao wanafunzi.
Pia Nigeria imekuwa ikishambuliwa na kundi la wanamgambo wa Boko Haram. Kundi ambalo limesababisha vifo vya watu wasiopungua 2,000 pamoja na kuwateka nyara wasichana wanafunzi wa shule ya sekondari ya bweni wasiopungua 200 huko Chibok huko kaskazini-mashariki mwa Nigeria.
Waziri Ngaisari alisema kongamano hilo litajadili sera mpya za kukabiliana na ugaidi.