Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Novemba 11, 2024 Local time: 16:55

Kenya tayari kupiga kura, polisi yaonya dhidi ya vitisho


Wagombea wakuu wa urais Kenya
Wagombea wakuu wa urais Kenya

Mamillioni ya wakenya watamiminika katika vituo vya kupigia kura Jumatatu asubuhi kupiga kura. Vituo vinafunguliwa kuanzia saa 12 asubuhi na kufungwa saa 11 jioni.

Wagombea wawili wanaongoza katika uchaguzi wa rais Kenya wanapambana bega bega katika utafiti wa hivi karibuni wa maoni ya watu. Waziri Mkuu Raila Odinga na mpinzani wake Makamu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta wote wamebashiri kushinda katika raundi ya kwanza. Lakini endapo hakuna mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50, raundi ya pili ya kura ya rais itafanyika mwezi Aprili.

Katika ujumbe kwa taifa Ijumaa, Rais Mwai Kibaki anayeondoka madarakani, alitoa wito wa uchaguzi wa amani na kuhimiza wagombea wote kukubali matokeo – ushindi au kushindwa.

Wakati huo huo, polisi nchini Kenya wanasema wana ripoti ya uwezekano wa vitisho. Msemaji wa polisi, Charles Owino, alisema kuna baadhi ya watu wanaopanga kuvaa sare za polisi na kushambulia raia katika maeneo ya mabanda Kibera na Mathare mjini Nairobi, na katika mji wa Kisumu, magharibi ya nchi. Owino anasema polisi watatumia kila nguvu waliyonayo endapo ni muhimu kuzuia vitisho vyovyote dhidi ya umma.

“Tuna jukumu la usalama humu nchini kwa hiyo ni wajibu wetu kukulinda (mwananchi). Na hatusemi kwa hofu, tunasema hivi kwa imani na ilani kwa sababu hatutaki watu wapoteze maisha.”

Kenya bado inakumbuka ghasia zilizotokea baada ya matokea ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambapo watu wapatao 1,100 waliuawa na wengine zaidi ya laki sita kupoteza makazi yao.

Kamishna wa tume ya uchaguzi, IEBC, Isaack Hassan, ametoa wito kwa wagombea kutumia njia ya kisheria kutatua matatizo ya matokea ya uchaguzi.

Zaidi ya Wakenya million 14 wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu. IEBC inatazamia huenda kukawa na changamoto katika upigaji kura. Wapiga kura mwaka huu wanachagua, pamoja na rais, maseneta, wawakilishi wa wanawake na wabunge. Vituo vya kupiga kura vinatazamia kufunguliwa saa 12 asubuhi na kufungwa saa 11 jioni, lakini IECB inasema watu watakaokuwa katika misitari wakati wa ufunguji vituo bado wataruhusiwa kupiga kura zao.
XS
SM
MD
LG