Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Februari 26, 2024 Local time: 11:08

Sifa za wakimbiaji Kenya mashakani kwa kashfa ya madawa


Rita Jeptoo wa Kenya akimaliza kwa ushindi mbio za Boston Marathon Aprili 15, 2013.
Rita Jeptoo wa Kenya akimaliza kwa ushindi mbio za Boston Marathon Aprili 15, 2013.

Rita Jeptoo amekanusha kutumia madawa ya kuongeza nguvu na chama cha riadha Kenya chasema vipimo alivyofanyiwa mkimbiaji huyo havikuwa na matokeo kamilifu

Mchezo wa riadha nchini Kenya umekumbwa na msukusuko baada ya mwanariadha wa kike Rita Jeptoo, mshindi wa mbio ndefu za Boston na Chicago hapa nchini Marekani, kudaiwa kuwa alitumiwa madawa ya kuongeza nguvu baada ya ushindi wake wa mbio ndefu za Chicago mwezi Oktoba.

Jeptoo ambaye amewahi kushinda mbio ndefu za Boston mara tatu inasemekana alikutwa mwilini na madawa ya kuongeza nguvu aina ya EPO - aina ya dawa aliyokutwa nayo mwendesha baiskeli bingwa wa Marekani Lance Armstrong ambaye mwaka 2012 alivuliwa ubingwa wa mbio za Tour de France alizoshinda kwa miaka saba mfululizo.

Jeptoo amekanusha kutumia madawa hayo, na chama cha riadha Kenya kinasema vipimo vya mkimbiaji huyo havikuwa na matokeo kamilifu. Lakini kashfa hiyo tayari inaleta msukosuko katika jamii ya wanariadha nchini humo. Kocha John Mwithiga ambaye amekuwa akifundisha riadha kwa miaka 25, ikiwa ni pamoja na wanaridha kadha waliowahi kuvunja rekodi za taifa, aliiambia Sauti ya Amerika kuwa tatizo la madawa limeanza kujitokeza hivi karibuni.

Mapema mwaka huu Professa Moni Wekesa alikuwa mwenyekiti wa kikosi cha kupambana na madawa ya kuongeza nguvu katika michezo na ripoti yao iliyowasilishwa mwezi uliopita ilikuwa na shutuma nyingi. Ripoti hiyo inasema Kenya haina hatua zozote za kudhibiti madawa ya kuongeza nguvu na kwamba madawa yenyewe yanapitakana kirahisi. Ripoti hiyo iliongeza kuwa wanariadha wa Kenya hawana maelezo kamili ya jinsi ya kuepuka madawa hayo.

Professa Wekesa anasema kwa hakika si haki kujaribu kuwaingiza wanariadha wote wa Kenya katika wimbi hilo, lakini uchunguzi wa matumizi ya madawa hayo hatimaye utakuwa ni matokeo mazuri kwa Kenya.

Mapema mwezi huu, waziri mmoja wa Kenya alikiri kwamba nchi hiyo ina tatizo la matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu, na kutangaza mipango ya kuanzisha idara ya kupambana na matumizi hayo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

XS
SM
MD
LG