Upatikanaji viungo

Jumanne, Desemba 06, 2022 Local time: 21:33

Kenya inatarajia uchumi wake kuimarika kwa asilimia 6 mwaka wa 2022.


Wafanyakazi wakitembea katikati ya shamba la chai Kericho, Kenya, Julai 24, 2020. Picha ya AFP.

Serikali ya Kenya imesema kuwa inatarajia uchumi wake kuimarika kwa asilimia 6% mwaka huu , baada ya kunawiri kwa asilimia asilimia 9.9% katika robo ya tatu ya mwaka wa kifedha wa 2021 pamoja na kuongezeka kwa mapokeo ya fedha kutoka raia wake wanaoishi Ughaibuni.

Serikali hiyo ya rais Kenyatta, baada ya kushuhudia ukuaji wa uchumi wake kupungua kwa asilimia 0.3 mwaka wa 2020/21 kutokana na athari ya maambukizi ya virusi vya Corona, pamoja na kiwango cha mfumuko wa bei za bidhaa kupanda hadi asilimia 5.4 mwaka huo kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona, imesema kuwa kuongezeka kwa mapokeo ya fedha kutoka kwa raia wake wanaoishi ughaibuni kumesababisha uchumi wake kuimarika kwa asilimia 6% mwaka huu.

Haya yalibainika Jumatatu wakati wa mkutano wa mashauriano kati ya kamati ya kitaifa ya utekelezaji wa maendeleo ya serikali, kupitia mawaziri mbalimbali na washirika wa maendeleo, mabalozi wa nchi za kigeni na wawekezaji nchini Kenya.

Uchumi wa Kenya uliongezeka kwa asilimia 5 mwaka wa 2019/2020.

Serikali inaeleza kuwa viashirio vikuu vya uchumi kuimarika kwa haraka kunatokana na maboresho ya ajabu yanayoshuhudiwa katika sekta ya huduma na viwanda.

Charles Karisa, mchambuzi wa masuala ya uchumi nchini Kenya anaeleza kuwa viashiria hivyo vya kutengamaa uchumi wa Kenya licha ya kuathiriwa na virusi vya Corona, kunatokana na mkakati ambao serikali imewekeza katika sekta mbalimbali za kiuchumi.

Lakini ameonyesha dukuduku kwa kufikia ukuaji wa uchumi kwa asilimia 6.

“Kwa maoni yangu, sidhani kwamba tunaweza kupata kiwango hicho cha asilimia 6, kwa sababu mwaka huu ambao ni mwaka wa uchaguzi, wawekezaji wanakuwa na mtazamo wa ‘subiri tuone’, Karisa amesema.

Serikali inakariri kuwa imezindua miradi yenye tija kwa uchumi wa Kenya na kuendelea kuwekeza katika sekta ambazo zina idadi nyingi ya raia wake, ikiwa ni nguzo katika ajenda nne kuu zake zinazowapa vijana fursa za ajira na kutengeneza kipato kwa familia, kutasaidia kupunguza athari ya virusi vya Corona kwa uchumi wake.

Ripoti hii imeandaliwa na mwandishi wa Sauti ya Amerika mjini Nairobi, Kennedy Wandera.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG