Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 08, 2023 Local time: 06:07

Katiba mpya ya Kenya na mfumo wa mahakama


Wakenya wakiwa na mabango yasemayo, "kura yangu ni nguvu yangu"
Wakenya wakiwa na mabango yasemayo, "kura yangu ni nguvu yangu"

Imewabidi mahasidi wa kisiasa kuunda ushirika wa vyama vyao ili kupata ushindi katika uchaguzi mkuu wa Machi ,4,2013

Tukiendelea na mfululizo wa makala zetu maalum juu ya uchaguzi mkuu nchini Kenya, tunaingia katika sehemu ya pili ya katiba mpya ya Kenya, na jinsi ilivyobadilisha kila sekta ya huduma za umma nchini humo ,ikiwemo mfumo wa mahakama na hususan uchaguzi ujao wa Machi nne .

Hadhi na sura ya Kenya ilitumbukia kizani baada ya uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka wa 2007. Mara baada ya matokeo kutangazwa, taifa hilo lilijikuta katika lindi la machafuko ya kikabila na maafa. Nchi ambayo ilikuwa mstari wa mbele kuunganisha mahasimu katika nchi jirani ilijikuta katika upande wa kuambiwa cha kufanya ili kuridhiana na kurejesha amani. Hofu ilitanda miongoni mwa Wakenya , na mbele ya jamii ya kimataifa hadhi ya Kenya ilishuka.

Katiba na mahakama Kenya
please wait

No media source currently available

0:00 0:06:26 0:00
Kiungo cha moja kwa moja

Ama kwa kweli hakuna aliyekuwa na uhakika ikiwa taifa hilo litaweza kujikwamua haraka na kuendelea kuwa kielelezo miongoni mwa dola za Afrika Mashariki. Lakini kama wahenga walivyosema, hakuna refu lisilo na ncha na hilo lilianza kubainika wazi baada ya Kenya kuidhinisha rasmi katiba mpya Agosti 27 mwaka wa 2010.

Tangu hapo Wakenya wameshuhudia mabadiliko makubwa kutokana na katiba hiyo ambayo wanasema inamwezesha mwananchi wa kawaida kuhisi kuwa ana sauti ya kusema; kutenda na kutetea haki yake, kinyume na nyakati za utawala uliokuwa wa katiba ya zamani waliyorithi kutoka kwa wakoloni wa Uingereza.Mwanasiasa na mchambuzi wa maswala ya kisiasa Maur Bwanamaka anasema, “Mimi kitu kikubwa ambacho nasherehekea ni katiba mpya ya Kenya.”

Mojawapo ya mafanikio makubwa ya katiba mpya ya Kenya ni kuweza kutofautisha majukumu ya mahakama, rais na bunge. Wakenya wanasema kutokana na katiba hiyo mfumo wa mahakama umekuwa una uwakilishi ufaao na viongozi kwenye mahakama wanazingatia katiba katika maamuzi yao. Mkereketwa wa kidemokrasia Patrick Ochieng anasema tangu kupitishwa kwa katiba mpya idara ya mahakama ndiyo imeweza kushikamana vyema zaidi na maagizo ya katiba.

Ingawa kuna mengi yanayotegemewa kunufaisha taifa hilo la Afrika Mashariki kutokana na katiba hiyo mpya, mtihani wa kwanza na mkubwa ni uchaguzi ujao wa Machi nne. Katika chaguzi za nyuma , wanasiasa walitegemea wingi wa wapiga kura kutoka kwa makabila yao lakini sasa imewabidi kuungana kwa sababu ni sharti wapate kura katika maeneo mbalimbali ya taifa hilo ili kupata ushindi.

Azma ya Wakenya kupata katiba mpya ilianza zamani. Nyakati za utawala wa rais mstaafu Daniel Moi kulikuwa na juhudi za kuwa na katiba mpya, lakini baada ya kuondoa kipengele maarufu (section 2a) cha kukubalia kuwe na vyama vingi vya kisiasa nchini humo, juhudi za kutaka katiba mpya zilizimwa na kushindikana.
Lakini chini ya utawala wa sasa wa rais Mwai Kibaki hayo yamewezekana kama anavyoeleza mwanaharakati wa kidemokrasia Patrick Ochieng. “Katika hatamu yake ya uongozi wa rais mwai Kibaki tumeweza kupata katiba mpya.”

Katika uchaguzi uliopita tume ya uchaguzi ilitupiwa lawama kubwa kwamba iliegemea upande mmoja. Hii sio mara ya kwanza kwa tume ya uchaguzi Kenya kuonekeana kuegemea upande mmoja. Chini ya utawala wa chama kimoja cha KANU maarufu kwa jina la utani kama Mama na Baba, ilikuwa bayana kwamba mgombea wa chama hicho atashinda uchaguzi.

Tume ya sasa inayosadikiwa na wengi kuwa itakuwa makini na huru, pia imepata changamoto na kuna maoni kuwa haikutoa elimu ya kutosha kwa umma kuelewa fika maswala mapya katika uchaguzi huu wa kwanza na wa aina yake ambao una viti vingi uwakilishi.

Inategemewa kutokana na msingi imara wa mfumo wa mahakama nchini Kenya chini ya mwongozo wa katiba mpya , maradhi sugu ya ufisadi yatatokomezwa hatua kwa hatua, lakini kuna maradhi mengine yanayohitaji tiba ya haraka nayo ni ukabila . Na kutokana na katiba mpya mahasidi wa kisiasa wamelazimika kuunda ushirika usio wa kikabila.

Hakuna shaka Wakenya wana matumaini makubwa kuwa taifa lao linaelekea kurejesha hadhi yake ya zamani na ikiwa katiba yao mpya itatekelezwa kikamilifu basi hamna shaka si katiba tu bali pia ni tiba ya kutegemewa.
XS
SM
MD
LG