Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 16, 2024 Local time: 19:45

Kampeni ya Cecilia Mnwanga yajikita katika kilimo, afya, elimu na lugha


Cecilia Augustino Mnwanga
Cecilia Augustino Mnwanga

Cecilia Augustino Mnwanga ni mwanamke wa pili kugombea urais nchini Tanzania kwa tiketi ya chama cha upinzani cha Demokrasia Makini. 

Cecilia ni jina ambalo tutalisikia sana katika viwanja vya kampeni za urais mwaka huu, akiwa ni mmoja kati ya wagombea wawili tu wanawake wanaowania nafasi ya juu ya uongozi.

Alipotangaza nia ya kuwania urais, Cecilian alibainisha wazi kuwa kampeni yake italenga katika masuala makuu manne ambayo yamo katika sera ya chama cha Demokrasia Makini.

Masuala ambayo ameyapa kipaumbele zaidi ni Kilimo, Afya, elimu na lugha.

Katika suala la kilimo alibainisha wazi kuwa hatua madhubuti ambazo zitakidhi mahitaji ya wakulima katika kuwa na kilimo cha kisasa zitachukuliwa ili kuongeza uzalishaji kilimo siyo tu katika upande wa biashara lakini pia katika uzalishaji chakula.

Suala la elimu na afya nayo atayashughulikia kwa dhati kabisa kwa sababu maeneo mengi ya vijijini yana changamoto kubwa sana katika Nyanja hizo na ili kusonga mbele kimaendeleo ni lazima kuwepo na mkakaati mzuri wa kuyashughulikia mapungufu yaliyopo katika elimu na afya.

"Lugha ya Kiswahili itapewa umuhimu mkubwa sana kwa vile lugha ndiyo kiini cha shughuli mbali mbali iwe za maendeleo, uchumi au siasa."

“Nitakuwa mtetezi wa kwanza mwanamke endapo nitachaguliwa kushika wadhifa wa uongozi. Nitaonyesha uadilifu mkubwa katika kazi yangu, lengo kuu likiwa ni kuhakikisha maeneo yenye mahitaji makubwa hasa ya vijijini yanatupiwa jicho na kupewa kila msaada unaohitajika,” amesema Cecilia mara tu baada ya kuchukua fomu ya kuwania urais.

Amesema ili kuonyesha kuwa anajali yale yanayo wakabili Watanzania hasa wa vijijini, kampeni zake zitalenga zaidi katika kuutumia usafiri maarufu katika maeneo ya vijijini nao ni basikeli, ili kuwaonyesha wengine kuwa tunafahamu changamoto zao na tuko katika juhudi za kuzitatua.

“Huwezi kuanza kuongea au kusoma, bila ya kupata mtu wa kukufundisha. Mimi nitakuwa ndiyo mwalimu katika kujaribu kutatua baadhi ya kero,” ujumbe wa Cecilia kwa wapiga kura wake.

XS
SM
MD
LG