Mtoto mmoja amefariki dunia na wengine 10 kujeruhiwa katika mlipuko uliotokea katika uwanja wa michezo karibu na shule ya msingi ya Kyaggwe Rd jijini Kampala Uganda Jumatano usiku.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi iliyokaririwa na vyombo vya habari nchini humo mtoto huyo alifariki dunia papo hapo baada ya kuokota kitu kinachodhaniwa ni bomu alipokuwa akicheza na wenzake uwanjani hapo.
Watoto hao wamelazwa katika hospitali ya serikali ya Mulago jijini Kampala , Sauti ya Amerika ilipata nafasi ya kuzungumza na mmoja wa wazazi, aliyekuwa akimwangalia mwanae hospitalini hapo Bw.Mbagoma Steven ambaye alieleza yaliomkuta mwanae Muzira Deus mwenye umri wa miaka 10 .
Daktari wa zamu wa hospitali hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Dennis alithibitisha kufariki dunia kwa mtoto mmoja.
Jiji la Kampala hivi sasa lina Polisi wengi na wanajeshi wanaofanya doria kuhakikisha usalama na mapema Jumatano asubuhi mkuu wa Polisi wa nchi hiyo Jenerali Kale Kaihura alithibitishia waandishi kwamba usalama umeimarishwa katika jiji hilo, lakini sauti ya Amerika ilimtafuta bila mafanikio simu yake ilikuwa imezimwa.