Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Mei 28, 2024 Local time: 04:51

Juhudi za kuzuia viongozi wa Kenya kwenda ICC


Majengo ya bunge la Kenya mjini Nairobi
Majengo ya bunge la Kenya mjini Nairobi
Mahakama ya kikatiba ya Kenya Jumatano ilianza kusikiliza ombi la kuzuia rais Uhuru Kenyatta na naibu rais William Ruto kuhudhuria vikao vya mahakama ya kimataifa ya ICC hadi pale watakapomaliza muhula wao wa miaka mitano kuongoza taifa hilo la Afrika Mashariki.

Waendesha mashataka wa ICC wanawashutumu rais Kenyatta na naibu rais Ruto kwa kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007 ambapo watu elfu moja na mia tatu waliuawa na maelfu kulazimika kuwa wakimbizi wa ndani.
Kesi dhidi ya bwana Ruto inategemewa kuanza kusikilizwa wiki ijayo.

Lakini Kundi la kutetea haki za kiraia la Kenya,The National Conservative Forum (NCF) liliwasilisha ombi katika mahakama ya kikatiba nchini humo, likisema kuwa kuondoka kwa viongozi hao wa Kenya kuhudhuria vikao vya kesi hizo huko The Hague kutaacha pengo la madaraka na mzozo wa kikatiba.

Kundi hilo linateta kuwa katiba ya Kenya inasema lazima rais na naibu wake wawe nchini ispokuwa katika mazingira yanayokubalika kisheria kwamba mmoja wao anaweza kuwa nje ya nchi kwa shughuli rasmi au za kawaida. Aidha NCF limefahamisha mahakama hiyo ya kikatiba kwamba katiba ya Kenya haijatoa mwongozo wowote au nafasi kwa rais wa nchi na naibu rais kumwachia mtu mwingine yeyote madaraka.

Akizungumza na Sauti ya Amerika, mkuu wa kundi hilo la haki za kiraia Jennifer Shamalla anasema imebainika wazi kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa wote,rais Kenyatta na naibu rais Ruto kuwa nje ya nchi kwa wakati mmoja. Shamalla anasema wakenya wana wasiwasi kuwa kutokuwepo nchini kwa viongozi hao wawili kutaibua hofu, hususan katika maswala ya kiusalama na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa wanamgambo wa Somalia, al-Shabab.

Anasema Kenya kuna uwezekano pia wa kuzuka mzozo wa kikabila, ambao huenda ukalitumbukiza taifa hilo katika duru nyingine ya ghasia. Kundi hilo linasema Kenya haitaki kufuata mkondo wa ghasia kama unaoshuhudiwa Misri, Libya au Syria.

Lakini wakosoaji wanasema ombi hilo kwa mahakama halina uzito wowote kwa sababu mahakama ya kikatiba ya Kenya haina uwezo wa kisheria juu ya mahakama ya kimataifa ICC. Navyo vyombo vya habari vya Kenya vinaripoti kuwa wabunge wa chama cha muungano wa Jubilee ulioko madarakani wanajiandaa kwa kikao maalum bungeni leo Alhamis kuzindua mdahalo juu ya Kenya kujiondoa kwenye mkataba wa Roma wa kuwa mwanachama wa mahakama ya kimataifa ya ICC.
XS
SM
MD
LG