Msemaji wa jeshi la Kenya kanali Cyrus Oguna alisema jumapili usiku kwamba jeshi hivi sasa linadhibiti kabisa soko la maduka ya kifahari mjini Nairobi la Westgate Mall ambako watu 68 waliuwawa na wanamgambo wa kisomali wa kundi la Al-shabab.
Anasema wengi wa mateka waliokuwa wamezuiwa ndani ya soko hilo kubwa wameokolewa lakini inavyoonekana washambuliaji wangali wanawashikiliwa mateka katika sehemu ya maduka na Jeshi la ulinzi la Kenya KDF linadhibiti jengo zima. Anasema idadi ya watu wanaoshikiliwa mateka haijazidi 10.
Uvamizi wa jengo hilo unaingia katika siku ya tatu jumatatu na jeshi linakadiria kuna kati ya washambuliaji 10 hadi 15.
Wanamgambo wa kundi la Kisomali la Al-Shabab wamedai kuhusika na shambulio hilo na kutishia jumatatu asubuhi kwamba watawauwa mateka wote ikiwa jeshi litaendelea kuwashambulia.
Shambulio hilo lilianza takriban saa sita mchana kwa saa za Kenya siku ya jumamosi katika soko la maduka ya kifahari la Westgate Mall na kusababisha vifo vya watu 68 na takriban 175 kujeruhiwa kufuatana na maafisa wa serikali.
Akilihutubia taifa Rais Uhuru Kenyatta katika hotuba yake kwa hamasa aliapa kusimama imara kupambana na kitisho cha ugaidi akiongeza kusema kwamba vikosi vya usalama vya Kenya vina nafasi nzuri ya kuwashinda waliohusika na shambulio hilo.
Akizungumza na Sauti ya Amerika-VOA mchambuzi wa masuala ya kiusalama na kijeshi Godwin Chilewa anasema huwenda kulikuwa na kasoro katika mfumo kamili wa usalama wa Kenya lakini ni vigumu kwa wakati huu kuvilaumu vikosi vya usalama hadi uchunguzi kufanyika.
Anasema tatizo kuu linaweza kuwa ni ukosefu wa mawasiliano kati ya idara mbali mbali za usalama na namna ya kukusanya habari za kijasusi na jukumu la raia vile vile.
Rais Barack Obama amezungumza na kiongozi mwenzake Uhuru Kenyatta na kutoa rambi rambi zake na kuahidi uungaji mkono wa Marekani katika juhudi za Kenya kupambana na ugaidi.