Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Septemba 29, 2023 Local time: 10:12

Wanajeshi wa Guinea Conakry wasema wameipindua serikali na kumkamata Rais Conde


Rais wa Guinea Conakry Alpha Conde.

Wanajeshi katika taifa la magharibi mwa Afrika la Guinea, Conakry, wamesema leo Jumapili kwamba wamemkamata rais wa nchi hiyo, Alpha Conde, na kuivunja serikali.

Video iliyotumwa kwa shirika la habari la AFP inawaonyesha wakieleza hayo. Hata hiyo, hadi tulipokuwa tukitayarisha ripoti hii, hali halisi kuhusiana na tukio hilo, bado haikujulikana bayana kwa kuwa serikali ya Conde pia, ilitoa taarifa ikisema kuwa shambulio la ikulu ya rais, lililotekelezwa na vikosi maalum, lilikuwa lkimedhibitiwa.

Awali, milio ya risasi ilisikika katikati mwa mji mkuu, Conakry, na wanajeshi walionekana barabarani, mashahidi waliliambia shirika la habari la AFP. Mwanadiplomasia mmoja mjini humo alitaja tukio hilo, kuwa jaribio la kuipindua serikali.

Hakukuwa na maelezo ya haraka kuhusu matukio yaliyoshuhudiwa katika eneo la Kaloum, kwenye mji huo wa Conakry, ambapo makao ya rais taasisi na afisi mbalimbali zipo.

Wakazi waliozungumza na AFP kwa njia ya simu walisema walisikia mfululizo wa milio ya risasi.

Wakizungumza kwa sharti la kutotambulishwa, mashahidi hao walisema waliwaona wanajeshi kwenye barabara za mji huo, ambao waliwataka wakazi kurudi manyumbani mwao na kusalia huko.

Guinea ni moja ya nchi maskini zaidi duniani, licha ya kuwa na raslimali nyingi za madini, na imekumbwa na mgogoro wa kisiasa kwa miaka kadhaa. Katika siku za nyuma, darzeni za watu waliuawa wakati wa maandamano, mara nyingi katika mapigano na vikosi vya usalama, na mamia kukamatwa.

Conde, mwenye umri wa miaka 83, alitangazwa kuwa rais mwezi Novemba mwaka jana, licha ya malalamiko ya udanganyifu wa uchaguzi kutoka kwa mpinzani wake mkuu Cellou Dalein Diallo, na wagombea wengine wa upinzani.

XS
SM
MD
LG