Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry amepanga Jumatano kuzungumzia dira yake namna mgogoro unaoendelea kati ya Israel na Wapalestina unaweza kutafutiwa ufumbuzi.
Suala hili ndilo analolipa kipaumbele Kerry tangu alipochukua wadhifa wa juu katika Wizara ya Mambo ya Nje February 2013. Lakini miaka yote hii ya mazungumzo, vikiwemo vipindi vya juhudi za juu zilizomfanya azunguke kwa ajili ya kutafuta suluhu za kidiplomasia, makubaliano hayakuweza kufikiwa juu ya suluhisho la kuwepo kwa mataifa mawili ambayo Kerry anaona ndio njia pekee yakufikia amani.
Kerry amebakiza mwezi mmoja kabla ya kumalizika kipindi cha utawala wa Rais Barack Obama, na iwapo makubaliano hatimaye yatafikiwa, hatokuwa yeye ndiye mwenye kuwekwa kwenye picha akitabasamu na kupeana mikono na viongozi wa-Israeli na wa-Palestina.
Hata hivyo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mark Toner amesema Jumanne kuwa Kerry anahisi ni wajibu wake kutumia muda uliobakia kupendekeza kile anachokiona kama ndio mustakbali wa kadhia ya mgogoro huu.
“Siku zote ni muhimu kujaribu kuendeleza mchakato wa amani, kuainisha dira zenye kujenga mustakbali, lakini pia kusisitiza ukweli kwamba hatujakata tamaa kukabiliana na hili tatizo, na hatutaki wa-Palestina au wa-Israeli wakate tamaa pia,” alisema Toner.
Kerry amesema katika hotuba yake zikibakia wiki mbili kama mwanadiplomasia wa juu wa Marekani kwamba yeye ana “matumaini” lakini kila mtu katika eneo la Mashariki ya Kati ana tambua kwamba dirisha la kufikia amani linakaribia kufungika.
Alisema hivi karibuni aliweza kuzileta pande mbili kushiriki katika mazungumzo ya amani kwa miezi tisa, lakini mchakato huo ulivurugika April 2014 bila ya pande hizo mbili kufikia makubaliano.
“Tunaamini kuwa wakati suluhisho la kuwa na mataifa mawili linakabiliwa na pingamizi, ni muhimu kuwashirikisha kujua ufahamu wa ndani wa matakwa ambayo tumeyafikia kwa pande zote mbili katika mashauriano ya kina katika miaka ya karibuni,” Afisa wa ngazi ya juu ya Wizara ya Mambo ya Nje alisema mapema kabla ya Kerry kuzungumza Jumatano.
Pingamizi mojawapo inayoyumbisha mashauriano haya ni kuendelea kwa Israel kujenga makazi katika maeneo ya wa-Palestina ambayo wana yaona ni sehemu ya taifa lao siku za usoni.
Suala hili lilirudi kwa kasi tena likachukua mstari wa mbele wiki iliyo pita pale uongozi wa Obama ulipojizuia kutumia kura ya turufu juu ya azimio la Umoja wa Mataifa lililo laani ujenzi wa makazi unaofanywa na Israel huko Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki.