India ilipiga marufuku uuzaji huo wa ngano wiki mbili zilizopita wakati kukiwa na wasiwasi kwamba wimbi la joto huenda liliharibu mazao nchini humo na kupelekea bei kupanda maradufu.
Waziri wa biashara na viwanda wa India Piyush Goyal amesema Jumatano kwamba maafisa wake walikuwa na wasiwasi kuhusiana na kudhibiti bei ya nafaka hiyo. Goyal wakati akihutubia kikao cha kimataifa cha uchumi mjii Davos Switzerland, alisema kwamba mataifa 22 ya Ulaya yameweka sheria za uuzaji wa nje ili kuhakikisha usalama wa ndani wa chakula, na kwamba mara kwa mara mataifa yamelazimika kuchukua hatua zisizo za kawaida ili kulinda maslahi ya watu wake.
Hatua ya India ya kupiga marufuku uuzaji wa nje wa ngano unalenga kudhibiti bei za ndani za bidhaa hiyo kwenye taifa hilo ambalo sawa na mataifa mengine linakabiliana na kushuka wa dhamani ya sarafu yake ambayo kufikia mwezi Aprili ilikuwa kwenye asilimia 7.8, kikiwa kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha miaka 8.
Serikali ya India mapema leo pia imetangaza kupunguza upelekaji wake wa sukari kwenye mataifa nje hadi tani milioni 10 pekee, hatua inayolenga pia kudhibiti bei za ndani. India ndiyo mzalishaji mkubwa zaidi wa sukari ulimwenguni na wa pili katika kuuza kwenye mataifa ya kigeni baada ya Brazil.
Kwenye mahojiano na shirika la habari la NDTV, mkuu wa shirika la kimataifa la fedha Kristina Georgieva amesihi India kubatilisha msimamo wake, akiongeza kwamba taifa hilo ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula ulimwenguni.