Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Oktoba 07, 2022 Local time: 02:39

Imam Rogo wa Kenya auwawa


Imam Mashuhuri wa Mombasa Aboud Rogo akiwa mahakamani

Imam huyo amekuwa akihusishwa na visa kadhaa vya ugaidi pamoja na umilikaji wa silaha bila vibali halali

Imam mmoja wa Kiislamu Aboud Rogo Mohamed raia wa Kenya ameripotiwa kuuawa Jumatatu asubuhi Agosti 27, 2012. Vyombo vya habari nchini Kenya vimeripoti kuwa Imam Rogo Mohamed aliuawa kwa kupigwa risasi na watu waliotoroka baadaye.

Shambulio hilo lilitokea katika eneo la Bamburi barabara kuu inayounganisha Mombasa na mji wa kitalii wa Malindi. Rogo alipigwa risasi akiwa ndani ya gari lake pamoja na jamaa zake wakielekea mjini Mombasa.

Habari zaidi zasema kuwa watu wawili waliokuwa ndani ya gari hilo wamepata majeraha akiwemo mke wa Rogo Mohammed. Imam huyo amekuwa akihusishwa na visa kadhaa vya ugaidi pamoja na umilikaji wa silaha bila vibali halali.

Mwezi mmoja uliopita aliandikisha taarifa katika kituo cha polisi mjini Nairobi, akidai kuwa zaidi watu 10 walijaribu kumteka nyara yeye na mwenzake Abubakar Shari Ahmed walipowasili Nairobi kuitikia wito wa kesi.

Mapema mwezi huu Rogo alikabiliwa na kesi juu ya mashtaka ya kukutwa na vilipuzi na silaha hatari nyumbani kwake. Kesi hiyo ilihamishwa kutoka mahakama za Nairobi na kuanza kusikizwa mahakamani mjini Mombasa.

Awali Imam Aboud Rogo Mohammed aliondolewa mashtaka mengine ya kuwa mshirika wa kundi la kigaidi linalohusika na kupanga mashambulizi katika eneo la Afrika Mashariki.
Ripoti ya upelelezi kutoka Marekani pia ilimtaja Imam huyo kuwa miongoni mwa watu wanaochunguzwa kwa tuhuma ya ugaidi. Maafisa wa usalama ndani na nje ya mji wa Mombasa wameanzisha uchunguzi kufuatia habari za mauaji ya Imam huyo wa Kiislamu.
XS
SM
MD
LG