Mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC imeanza kusikiliza kesi ikiwa waziri wa zamani wa Ivory Coast na mwanaharakati wa vijana, Charles Ble Goude anastahili kukabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu. Ble Goude ni mshirika wa karibu wa rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, anashutumiwa kuwa mhusika mkuu katika ghasia ambazo zilifuatia kushindwa kwa Gbagbo katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2010 na juhudi zake za kutaka kuendelea kukaa madarakani.
Akiwa amevalia suti ya kijivu, Charles Ble Goude alisikiliza kwa makini hoja ya ufunguzi wa mashtaka yake iliyosomwa na jaji, Silvia Fernandez de Gurmendi. “Kesi ya wiki hii katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC ni ya kuchukua uwamuzi kama Ble Goude mwenye umri wa miaka 40 afunguliwe mashtaka au la, kwa makosa manne ya uhalifu dhidi ya binadamu, ikiwemo mauaji, ubakaji na kutenda mateso.
Suala kuu hapa; ni ghasia katika nchi yake ya Ivory Coast kati ya mwezi Novemba 2010 na April 2011, baada ya uchaguzi wa kiti cha rais kilichohusika rais wa muda mrefu Laurent Gbagbo na mgombea Alassane Ouattara, ambaye ndio Rais wa sasa nchini humo. Takribani watu 3,000 waliuwawa katika ghasia hizo ambazo zilizuka baada ya Gbagbo kukataa kukubali matokeo ya kushindwa kwenye uchaguzi huo.
Ble Goude alikuwa mshirika wa karibu wa Gbagbo na mkewe Gbagbo, Simone. Anajulikana kama mtu mwenye ushawishi mkubwa aliyeongoza wanamgambo wa kundi linalomuunga mkono Gbagbo liitwalo “Youth patriots” ambalo linalaumiwa kwa kampeni za ghasia baada ya uchaguzi dhidi ya wafuasi wa Ouattara. Yeye anakanusha tuhuma hizo.
Akizungumza katika kikao hicho cha ufunguzi, mwendesha mashtaka mkuu wa ICC, Fatou Bensouda alielezea jinsi matukio ya Novemba mwaka 2010 yaliofuatia mzozo wa matokeo ya uchaguzi wa rais namna yalivyotendeka. “mnamo siku chache tu, nchi ya Ivory Coast ilibadilika kutoka ile nchi ya amani ya watu wamepiga kura kwa njia ya kidemokrasia na kutumbukia kwenye dimbwi la ghasia zilizosababisha machafuko na mgawanyiko”.
Bibi Bensouda aliendelea kusema kwa upande wa vitendo vya mauaji ya aina hii huwenda bwana Ble Goude akafunguliwa mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu na tutaomba mahakama kumfungulia mashtaka hayo”
Mwanzoni mwa mwezi huu ICC ilidhinisha kufunguliwa mashtaka dhidi ya Gbagbo mwenyewe kwa uhalifu dhidi ya binadamu pamoja na ghasia zilizohusiana na matukio kama hayo mwaka 2010 hadi 2011 na kumfanya kuwa rais wa kwanza aliyeondoka madarakani kukabiliwa na mashtaka kwenye mahakama hiyo yenye makao makuu yake The Hague.
Kesi yaa Ble inasikilizwa hadi Alhamis. Hapo tena Majaji watakuwa na siku 60 za kuamua kama wamfungulie kesi au la.