Umoja mataifa na makundi ya kutetea haki yameitaka Misri kusitisha ukandamizaji wa wanaharakati wa haki na kuacha kuwawekea vipingamizi kwenye shughuli zao.
Mashirika 14 ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Human Rights Watch na Amnesty International, yamesema kuwa maafisa wa Misri wanapaswa kuacha kuwaita wanaharakati wa kutetea haki kwenda kuwahoji, kuwapiga marufuku kusafiri na kujaribu kuzuia mali zao binafsi na za familia zao.
Mashirika hayo yanasema, maafisa wanapaswa kusitisha ukandamizaji wa makundi hayo na kutupilia mbali uchunguzi ambao unaweza kutishia watetezi wa haki za binadam kupewa kifungo cha hadi miaka 25 jela.
Makundi ya kutetea haki mara kwa mara yameshutumu idara za usalama za Misri kwa kuwaweka kizuizini kinyume cha sheria, wanaharakati kupotea na kadhalika mateso kwa wafungwa.
Said Bourmedouha, naibu mkurugenzi wa Amnesty International kwa Mashariki ya kati na Afrika kaskazni, anasema makundi ya kiraia nchini misri yanatendewwa kama maadui wa seriklai, kuliko kuonekana kuwa ni washirika wa mageuzi na maendeleo.
Marekani na mataifa ya Ulaya yamelaani vitendo wanavyofanyiwa watetezi wa haki za binadam na wamewaondowa raia wao kadhaa ambao wametishiwa kukamatwa.