Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Julai 15, 2024 Local time: 08:39

Hukumu ya Lubanga kutolewa Jumanne


Thomas Lubanga mwenye kofia akiwa kwenye chumba cha mahakama na mawakili wake huko The Hague
Thomas Lubanga mwenye kofia akiwa kwenye chumba cha mahakama na mawakili wake huko The Hague

Waendesha mashtaka wanaangalia hukumu inayostahili kwa Lubanga kati ya miaka 30 hadi kifungo cha maisha jela

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC inapanga kutoa hukumu yake ya kwanza Jumanne katika kesi inayomhusisha mbabe wa kivita Thomas Lubanga wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Lubanga alikutwa na hatia ya uhalifu wa vita mwezi Machi kwa kutoa mafunzo na kuwatumia wanajeshi watoto wakati wa mapigano huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC mwaka 2002 na mwaka 2003.

Kundi la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilisema Jumatatu kuwa hukumu ya Lubanga ni muhimu sio tu kwa waathirika wake, lakini pia ni onyo kwa wale wanaowatumia wanajeshi watoto duniani kote.

Hukumu ya Lubanga itakuwa ya kwanza kutolewa na ICC tangu mahakama hiyo ilipoanzishwa muongo mmoja uliopita.

Waendesha mashtaka wa mahakama wanaangalia hukumu inayostahili kwa Lubanga ambayo inaweza kuwa kati ya miaka 30 hadi kifungo cha maisha jela.

Jopo la majaji lilitangaza kwa pamoja kwamba Lubanga alitoa mafunzo kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 kupambana kwa kutumia silaha ili kulilinda kundi lake.

Amekuwa kwenye kizuizi cha ICC huko The Haque tangu mwezi machi mwaka 2005.

Wakati huo huo mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC inamtafuta kiongozi mwingine wa wanamgambo wa Congo, Bosco Ntaganda, ambaye inasemekana alikuwa kiongozi wa cheo cha tatu katika jeshi la Lubanga. Wanajeshi wanaomtii Lubanga waliondoka katika jeshi la Congo mwanzoni mwa mwaka huu na walianza kufanya uasi unaoendelea huko mashariki karibu na mpaka na Uganda.


XS
SM
MD
LG