Rais wa Marekani Barack Obama ameamuru ongezeko la idadi ya wanajeshi kutoka kikosi maalum cha operesheni za kijeshi za Marekani kwenda Syria na kuyasihi mataifa ya Ulaya kuchangia kwenye ushirika unaopambana na kundi la Islamic State.
Akiongea kwenye maonyesho ya biashara leo Jumatatu huko Hannover, Ujerumani, Obama amesema kiasi cha wanajeshi 250 wa ziada watajiunga na timu ya wanajeshi 50 wa Marekani walioko nchini Syria.
"Utalaamu wao umekuwa ni muhimu sana kwa majeshi ya ndani ambayo yamewasukuma kutoka maeneo muhimu yaliyokuwa yakikaliwa na ISIL," amesema Obama.
Mapema mwezi huu, Marekani imetangaza upelekaji wa wanajeshi 200 wa ziada na helikopta za kivita aina ya Apache nchini Iraq, ambako watayasaidia majeshi ya serikali kuchukua tena maeneo yaliyokuwa yamekamatwa na ISIL.